TAMBO ZA NANI ZAIDI, SIMBA NA YANGA KOMBE LA KAGAME KUMALIZWA LEO

TAMBO, ngebe na majingambo ya nani zaidi kati ya Yanga na Simba zitajulikana  leo katika mchezo wa fainali  za michuano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati ‘Kagame Castle Cup’, kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hii ni mara ya tatu kwa timu hizo kukutana katika hatua ya fainali ya michuano tangu ilipoanzishwa mwaka 1974 ambapo, mwaka 1975 zilikutana kwa mara ya kwanza katika fainali iliyopigwa kwenye uwanja wa Amaan, Zanzibar, ambapo Yanga ilitwaa ubingwa baada ya kushinda mabao 2-0.
Timu hizo zikakutana tena katika fainali iliyofanyika kwenye uwanja wa Amaan, Zanzibar mwaka 1992 ambapo Simba ililipiza kisasi kwa kushinda kwa penalti 5-4 baada ya sare ya bila kufunguna ndani ya dakika 120.
Kwa hali hiyo, kila timu itacheza kufa kupona katika mechi hiyo ili kushinda na kuandika historia ambapo kihistoria Simba inaongoza kwa kutwaa taji la michuano hiyo mara sita huku Yanga ikiwa imetwaa mara tatu.
Wakati Simba ilianza kutinga hatua hiyo baada ya kuifunga kwa penalti 5-4 El Merreikh ya Sudan baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga nao ilitinga fainali baada ya kuifunga St.George ya Ethiopia  kwa penalti 5-4, baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Mechi hiyo ta fainali imekuwa gumzo kila kona ya nchi, ambapo mashabiki pamoja na viongozi wa timu zote kila mmoja ametamba timu yake kuibuka mshindi leo, hali ambayo inafanya joto la mchezo huo lizidi kupanda kwa kasi kadiri muda unavyosogea.

Comments