SIMBA SC YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA KAGAME



MABINGWA mara sita wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame’ Simba ya Dar es Salaam, jana walifanikiwa kutinga robo faini ya kombe hilo baada ya kuichapa Etincelles ya Rwanda kwa mabao 2-0, katika mechi iliyopigwa kwenye dimba la taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo iliyochezeshwa vema na mwamuzi Loluseghed Michael wa Eritrea, bao la kwanza la Simba lilifungwa na Haruna Moshi ‘Boban’ aliyemalizia mpira wa kichwa uliopigwa na Mohammed Banka na kugonga mwamba kisha kurudi uwanjani na kumkuta Boban aliyeutumbukiza wavuni.
Kipindi cha pili Simba ilikianza kwa nguvu ikipeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Etincelles, lakini washambuliaji wake walikosa mbinu za kuupenya ukuta mzito wa wapinzani wao.
Kutokana na wachezaji wa timu ya Etincelles wote kurudi nyuma kuzuia, Simba walilazimika kusubiri hadi dakika 74, baada ya mtokea benchi Musa Mgosi kuwafungia bao la pili akimalizia pasi ya Patrick Mafisango.
Kipigo hicho kimewafanya Etincelles kuyaaga rasmi mashindano hayo, kutokana na kupoteza mechi zote hatua ya makundi, huku ushindi ukiwavusha Simba hadi hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Comments