SIMBA NA BUNAMWAYA, YANGA NA RED SEA

MATOKEO ya mechi za mwisho hatua ya Makundi Kombe la Kagame Julai 3 yameamua robo fainali iwe kati ya Simba na Bunamwaya ya Uganda, huku Yanga ikivaana na Red Sea ya Eritrea.
Katika michezo iliyofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam yote ikihusisha Kundi A, Simba ilitoka 0-0 na Red Sea ya Eritrea, wakati Vital ‘O iliifunga Zanzibar Ocean View bao 1- 0.
Kwa hesabu hizo, Simba imemaliza ikiwa ya kwanza Kundi A ikiwa na pointi nane, Red Sea yenye pointi saba sawa na Vital ‘O ya Burundi.
Timu zote hizo zinalingana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, zote zikiwa na faida ya mabao mawili, lakini Red Sea imefunga mabao matano, wakati Vital ‘O imefunga mabao manne.
Kulingana na taratibu za Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), timu tatu za Kundi A, pamoja na timu mbili za juu Kundi B na mbili za Kundi C zitacheza robo
fainali pamoja na timu moja itakayokuwa na uwiano mzuri wa pointi kutoka Kundi B ama C.
Simba kwa kuongoza kundi lake itavaana na timu iliyopenya kutokana na kuwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa ambayo ni Bunamwaya ya Uganda na mchezo huo utafanyika kesho.
Mchezo mwingine utakaofanyika kesho utahusisha mshindi wa pili Kundi B ambaye ni El Merreikh ya Sudani itakayocheza na Ulinzi, mechi zote zikichezwa kesho.
Yanga iliyoongoza Kundi B ikiwa na pointi saba itacheza na mshindi wa pili Kundi A ambaye ni Red Sea, huku mshindi wa tatu Kundi A ambaye ni Vital ‘O ikicheza na mshindi wa kwanza Kundi C ambaye ni St, George ya Ethiopia. Mechi hizo zitachezwa kesho.
Nusu fainali itafanyika Alhamisi ikihusisha mshindi wa mechi kati ya Simba na Bunamwaya na ile ya El Merreikh na Ulinzi na siku inayofuata nusu fainali nyingine itakuwa kati ya mshindi wa mechi ya Yanga na Red Sea atavaana na mshindi wa mechi ya Vital ‘O na St. George.
Katika mchezo kati ya Simba na Red Sea, washambuliaji wa Simba walikosa nafasi nyingi za kufunga kwa kupiga mipira hovyo langoni.
Mussa Mgosi, Haruna Moshi, Shija Mkina na Rajabu Isihaka kwa nyakati tofauti walipata nafasi za kufunga, lakini umaliziaji haukuwa mzuri.
Kwa upande wa Red Sea yenyewe muda mwingi ilikuwa ikilinda lango zaidi na nafasi chache ilizopata Aron Zekarias, Yakob Amanuel na Abrahm Tedros walishindwa kuzitumia.
Timu ya Zanzibar Ocean View iliyokuwa Kundi A ambayo ilianza kwa makeke hatua za makundi kwa kushinda michezo yake miwili ya awali imejikuta ikiwa miongoni mwa timu tano zilizofunga virago kurejea nyumbani.
Nyingine ni Etincelles na APR za Rwanda, Ports ya Djibout, Elman ya Somalia.

Comments