SERIKALI YASHANGAZWA KUTOWASHWA JENERETA UWANJA WA TAIFA



NAIBU Waziri wa Nishati na Madini,  Adam Malima (Pichani kushoto) ameeleza kushangazwa kutotumiwa kwa jenereta za dharura katika Uwanja wa Taifa wakati wa mechi ya fainali ya Kombe la Kagame dhidi ya Simba Jumapili iliyopita.
Malima alitoa maelezo hayo bungeni jana, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim, aliyehoji serikali inawaambia nini Watanzania kutokana na kukatika kwa umeme, wakati Yanga ikikabidhiwa kombe la ushindi katika michuano hiyo.
Akijibu swali hilo, Malima alisema, siku hiyo umeme ulikatika katika kituo cha umeme Kurasini, lakini uliporudi maeneo ya uwanja huo kulikuwa na hitilafu.
“Kutokana na hali hiyo, umeme katika maeneo mengine ulirudi, lakini upande wa Uwanja wa Taifa haukurudi, lakini pale uwanjani kuna jenereta za dharura, nashangaa kwa nini hazikuwashwa,” alisema Malima.
Hata hivyo, alisema suala hilo wanaendelea kulishughulikia ili liweze kupatiwa ufumbuzi.

Comments