SAID FELLA AGEUKIA TAARAB RASMI


KIONGOZI wa kundi la muziki wa kizazi kipya la TMK Wanaume Family la Temeke jijini Dar es Salaam, Said Fella, ambaye kwa sasa ameamua kushika ‘mic’, amesema kuanzia sasa atapanda jukwaani kuimba ili kuinadi albamu yake ya taarabu.
 Fella alisema kuwa ameamua rasmi kuanza kuinadi albamu hiyo ambayo bado hajaipa jina, tayari akiwa amekamilisha nyimbo tano.
Alisema, anajipanga kuandaa maonyesho ambayo ataimba ‘Live’ akiwa na bendi yake mpya ya Mkubwa na Wanawe, aliyoianzisha hivi karibuni.
Fella alisema kuwa mbali ya kuandaa maonyesho hayo, pia atashirikiana katika shoo zitakazozinduliwa na makundi mengine ya taarabu ili wapenzi wa muziki huo waanze kumuona na kuzisikia kazi zake kabla hajaziingiza sokoni.
“Mkubwa kuanzia sasa nimeamua kushika mic na ninaanza kuimba kuzinadi nyimbo za albamu yangu ya taarab, nitaandaa maonyesho na pia nitashiriki kwenye maonyesho ya makundi mengine ya taarabu na pia kama mtu atanihitaji katika onyesho lake, tutajadili mambo ya maslahi, nikiridhika nitaimba,” alisema Fella.
Katika albamu yake hiyo, Fella amewashirikisha wakali wa mipasho wakiwamo Hassan Kumbi, Maua Tego, Isha Ramadhani ‘Isha Mashauzi’ na malkia wa mipasho nchini, Khadija Omari Kopa.

Comments