NI MORO NA KIGOMA FAINALI COPA COCA COLA

FAINALI ya michuano ya vijana ya Copa Coca-Cola ni kati ya Mkoa wa Kigoma na Morogoro.

Kitendawili hicho cha timu ya pili itakayocheza fainali kiliteguliwa Juni 30 jioni, wakati Morogoro ilipoifunga Kilimanjaro mabao 2-1 katika mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo kwenye Uwanja wa Karume.
Juni 29 Kigoma iliifunga Temeke bao 1-0, hivyo kutangulia fainali, ambayo itafanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Temeke na Kilimanjaro zitawania mshindi wa tatu Jumapili asubuhi. Kilimanjaro ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 16 mfungaji akiwa Tumaini Tenance kwa penalti, baada ya mabeki wa Morogoro kumchezea madhambi.
Bao hilo lilionekana kuwazindua Morogoro na kuongeza kasi, lakini umaliziaji haukuwa mzuri, huku pia Kilimanjaro nayo ikipoteza nafasi nyingi za kufunga.
Morogoro ilisawazisha bao dakika ya 66 mfungaji akiwa Basil Rashid kutokana na mpira uliokuwa ukizagaa baada ya kuwashinda mabeki wa Kilimanjaro.
Bao la ushindi lilifungwa dakika ya 75 na Abdul tena hivyo kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Morogoro kuona timu yao ikitinga fainali.



Comments