BASATA YATOA ELIMU YA VVU KWA WASANII

Taji Liundi akiwaonesha Wasanii na wadau wa Sanaa jinsi Virusi vya UKIMWI vinavyopenya kwenye damu na kusababisha mtu kudhoofu. Kulia kwake ni Kaimu Mratibu wa Programu ya Jukwaa la Sanaa, Bi.Agnes Kimwaga.
Msanii maarufu wa Sanaa ya Uchoraji Mohamed Raza akiuliza na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimabali kuhusu VVU.
Mdau akimuuliza muelimishaji rika juu ya matumizi ya Kinga na nafasi yake katika kukinga maambukizi ya VVU.
Sehemu ya Wadau wakimsikiliza muelimishaji rika Taji Liundi. Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kupitia programu yake ya kila wiki ya Jukwaa la Sanaa limetoa elimu kwa wadau wa sanaa kuhusu virusi vinavyosababisha UKIMWI na jinsi vinavyoweza kuathiri mwili wa binadamu.
Akizungumza kwenye program hiyo, muelimishaji rika na kamishna mstaafu wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini, Taji Liundi alisema kwamba,wasanii ni kada inayoathirika sana na janga hili hivyo elimu hiyo ni muhimu kwa wao kujikinga na kuwakinga mashabiki wao.
“Umaarufu wa wasanii unaletwa na mashabiki na kazi yao ni ya muingiliano mkubwa kiasi kwamba wanatakiwa kuwa makini ili mwisho wa siku wasipukutuke na janga hili. Wanapaswa kuzingatia elimu kama hizi na hata kubuni kazi zenye kuzingatia haya” alisema Taji Liundi.
Awali akitoa elimu kwa wadau wa sanaa Taji alisema kwamba,wasanii wengi wamekuwa wakijikuta kwenye vishawishi vya kufanya vitendo vya ngono na watu wasiyowafahamu na waliokutana nao kwa mara ya kwanza kwenye maonyesho hali ambayo inahatarisha afya zao.
Aliongeza kwamba, umaarufu, matamanio na kuamini bila kutumia vipimo ndivyo vimekuwa vikiwaweka watu wengi hususan wasanii wenye muingiliano mkubwa na jamii katika mazingira hatari ya kuambukizwa VVU.
Alizidi kueleza kwamba, kwa sasa hakuna kampeni zinazolenga kupambana na janga hili kama ilivyokuwa zamani ambapo kampeni kama za ISHI zilisaidia kutoa elimu pana kwa jamii hivyo kutoa wito kwa wasanii kutumia fursa kama za Jukwaa la Sanaa katika kupata elimu hii muhimu.
Baraza la Sanaa limekuwa likiendesha program maalum ya Afya kwa wadau wa Sanaa hususan wasanii kila baada ya miezi mitatu na tayari wasanii na wadau wapatao 200 wameshapewa elimu ya VVU na kupima afya zao.

Comments