MWAMUZI AFUNGIWA MIAKA MITANO


Kamati ya Rufani ya TFF iliyokaa Julai 23 mwaka huu imesikiliza rufani 
iliyokatwa na Mwamuzi wa Daraja la Kwanza, Kamwanga Tambwe. Baada ya kuangalia 
nyaraka zilizotolewa kwenye kamati, kumsikiliza na kumhoji, kamati imefikia 
uamuzi ufuatao;
 
Kamati ya Rufani imeona rufani hii haina msingi, na hivyo kutoa adhabu 
zifuatazo;
 
1.   Kumfungia Mwamuzi Kamwanga Tambwe kutojihusisha na masuala ya mpira wa 
miguu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Oktoba 20, 2009 kulingana na Ibara ya 
45 (ii) ya Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikisomwa pamoja 
na Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) Ibara 
ya 62(ii).
 
2.   Fedha shilingi laki mbili (200,000/-) zilizohusishwa na rushwa katika 
shauri hili, kufuatana na kifungu 62(iv) cha Kanuni za Nidhamu za FIFA zibaki 
TFF kwa shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu.
 
Imesainiwa na Wajumbe wa Kamati ya Rufani;
 
Prof. G. Mgongo Fimbo                                                                                             - Mwenyekiti
Dk. Ong’wanuhama Kibuta                                                                                     - Makamu Mwenyekiti
Lt. Kanali mstaafu Idd Kipingu                                                                                - Mjumbe
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Jamal Rwambow           - Mjumbe
Henry  Tandau                                                                                                             - Mjumbe
 
Taarifa za nyongeza (background information);
Tambwe na wenzake walifungiwa maisha na Kamati ya Mashindano ya TFF kwa tuhuma 
za kupokea rushwa kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Majimaji ya Songea 
na Mtibwa Sugar ya Morogoro iliyochezwa mwaka 2009. Awali walikata rufani Kamati 
ya Nidhamu ya TFF ambayo iliwapunguzia adhabu hiyo hadi miaka mitatu. Tambwe kwa 
upande wake hakuridhika na uamuzi huo, hivyo kukata rufani Kamati ya Rufani ya 
TFF.
 
Boniface Wambura 
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Comments