MGOSI AENDA KUCHEZA KWA RIDHAA DC MOTEMA PEMBE

KLABU ya soka ya Daring Club Motema Pembe (DCMP) ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imeliandikia barua shirikisho la soka Tanzania (TFF) ikiomba hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) ya mshambuliaji wa Simba, Musa Hassan Mgosi.

Hata hivyo, DCMP kupitia Shirikisho la vyama vya mpira wa miguu vya nchi hiyo (FECOFA) limeomba ITC ya Mgosi kama mchezaji wa ridhaa.

Ofisa habari wa Tff, Boniface Wambura alisema kwamba klabu hiyo imedai kuwa  imeshakubaliana na wenzao wa Simba katika suala hilo.

Alisema, kabla ya kufanya hivyo, watawasiliana kwanza  na Simba ili kuona kama kweli wamekubaliana kuhusiana na uhamisho wa mchezaji huyo na ndipo waweze kutoa hati hiyo.

Kabla ya kwenda kujaribu bahati yake DCMP, Mgosi alikuwa ni mmoja ya wachezaji ambao walikuwa kwenye orodha ya kuhamishwa kwa mkopo katika klabu nyingine za ligi kuu Tanzania Bara ili aweze kuzichezea katika msimu mpya wa ligi hiyo unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20.

Simba ilifikia hatua ya kuwaondoa wachezaji hao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kushuka viwango pamoja na utovu wa nidhamu ambao umechangia kuinyima timu mataji ya ligi kuu ya Vodacom pamoja na Kagame.

Wachezaji ambao Simba imewatoa kwa mkopo ni pamoja na Mohammed banka, Mohammed Kijuso, Haruna Shamte (Villa Squad), Ali Ahmed Shiboli (Kagera Sugar), Aziz Gilla, Mbwana Bakari (Coastal Union), Meshack Abel (Ruvu Shooting).

Wengine ni Juma Jabu, Andrew Kazembe, Paulo Terry na Godfrey Wambura ambao wamepelekwa Moro United.

Comments