KUWAONA WATOTO WA JULIO, SHELISHELI 10,000

Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 23 (U23) itacheza mechi mbili 
za kirafiki za kimataifa dhidi ya timu ya Taifa ya Shelisheli kwenye Uwanja wa 
Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Kaluta jijini Arusha. Kiingilio cha chini katika 
mechi hizo kitakuwa sh. 3,000.
 
Kwa jukwaa kuu kiingilio kitakuwa sh. 10,000 wakati kiingilio kingine ni sh. 
5,000. Timu ya Shelisheli tayari iko jijini Arusha ambapo iliwasili Julai 22 
mwaka huu mchana ikitokea Nairobi, Kenya tayari kwa mechi hizo.
 
Mechi ya kwanza itachezwa Julai 27 mwaka huu, wakati nyingine itakuwa Julai 29 
mwaka huu. Mechi zitaanza saa 10 jioni, na Shelisheli inatarajia kuondoka nchini 
kurejea kwao Julai 30 mwaka huu kwa kupitia Nairobi.
 
U23 ambayo iko chini ya kocha Jamhuri Kihwelo imeondoka leo asubuhi (Julai 25 
mwaka huu) kwenda Arusha. Itafanya mazoezi yake ya kwanza jijini humo leo jioni 
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Kaluta.
 
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen pia yuko na timu hiyo akitoa ushauri wa 
kiufundi baada ya kuongeza wachezaji Haruna Moshi ‘Boban’ wa Simba, Juma Seif 
Kijiko wa Yanga na mfungaji bora wa michuano ya Kili Taifa Cup, Gaudence 
Mwaikimba wa Moro United kwa lengo la kuangalia viwango vyao kwenye mechi hizo 
ili kuona kama watamfaa kwenye kikosi cha Stars.
 
Baada ya mechi hizo, Julai 30 mwaka huu jijini Arusha, Poulsen atataja kikosi 
cha Stars ambacho kitaingia kambini Agosti 2 mwaka huu kwa ajili ya mechi ya 
kirafiki ya kimataifa dhidi ya Palestina. 

 
Taifa Stars inatarajia kuondoka Agosti 7 mwaka huu kwenda Palestina kwa ajili ya 
mechi hiyo itakayochezwa Agosti 10 mwaka huu jijini Ramallah. Timu itarejea 
Agosti 11 mwaka huu.

Comments