KIPINGU AWASHUKIA NYOTA WANAOKACHA MASOMO NA KUKIMBIA SIMBA, YANGA

Kanali Idd Kipingu,
MWENYEKITI wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) , Kanali Idd Kipingu, amewashukia baadhi ya wachezaji nyota wa klabu kongwe za Simba na Yanga ambao wameamua kukataa kuendelea na masomo na kujikita kwenye soka.

Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo ya wiki mbili ya mchezo wa mpira wa kikapu, Kipingu, alisema wachezaji hao wamefanya kosa kubwa sana kuacha masomo na kujikita kwenye mpira, kwakuwa hata huko walipo bado hawana uhakika wa kuendesha maisha yao.

“Wamefanya makosa makubwa kuacha masomo, walichotakiwa ni kuendelea huku wakicheza soka kwakuwa haya mambo yanaweza kwenda sambamba bila kuathiri programu zao za kila siku shuleni,” alisema Kipingu.

Alisema kuwa shule inaambatana na michezo, hivyo aliwataka wachezaji wote waliopo kwenye masomo kuhakikisha wanazingatia vitu vyote viwili, kwakuwa vina faida, ambapo alitaka uigwe mfano wa Chuo cha Mamb Canada ambacho kinafanya vizuri katika elimu na michezo.

Kipingu alimpongeza mchezaji aliyepata udhamini kwenda kusoma Chuo cha Mamb kilichopo Canada, Alpha Kisusi, ambaye amechaguliwa na kocha aliyekuwa anatoa mafunzo ya mchezo huo kutoka chuo hicho ambapo alimtaka kuzingatia masomo na michezo atakapofika huko.

Naye kocha kutoka chuo hicho, Peter Benoite, alisema amefurahishwa na wachezaji wote aliokuwa akiwapa mafunzo ambapo alisema mwakani atakapokuja atapata wachezaji wazuri zaidi ya mwaka huu kwa kuwa watakuwa wamejiandaa vya kutosha.

Kocha huyo alikuwa akitumia vigezo mbalimbali katika kuchagua wachezaji watakaojiunga na timu anayoifundisha ya chuo hicho vikiwamo kuwa na uwezo kimasomo na kimichezo hasa basketball.

Comments