K-MONDO SOUND KUWABURUDISHA WALIOWAHI KUSOMA SEKONDARI YA KISUTU JULAI 17



Bendi ya muziki wa dansi ya K-Mondo Sound inatarajia kuwatumbuiza wanafunzi mbalimbali waliowahi kusoma katika shule ya msingi Kisutu iliyopo mjini Dar es Salaam.

Kiongozi wa bendi hiyo, Richard Mangustino amesema mjini Dar es Salaam kuwa onyesho hilo litafanyika Julai 17 kwenye hoteli ya Giraffe kuanzia saa 12 jioni.
“Mmoja wa wanafunzi waliosoma Kisutu alitueleza kuwa wanataka kukutana na kukukumbushana mambo mbalimbali pamoja na kutengeneza umoja wao, awali walikutana mara ya kwanza Januari mwaka huu wakaazimia kukutana tena shuleni kwao lakini haikufanyika sasa wameamua kurudi Giraffe na sisi tumewaandalia burudani ya nguvu,” alisema.
Alisema wanafunzi hao ni wale waliosoma kati ya mwaka 1980 hadi miaka ya tisini wakati shule hiyo ikiwa chini ya serikali baada ya kutaifishwa kutoka kwa jumuiya ya wahindu.
Awali walionza kukutana ni wanafunzi waliomaliza Kisutu mwaka 1990 lakini watu wengi zaidi wakajiunga katika kundi hilo ambapo pia taarifa mbalimbali zinapatikana katika mtandao wa Facebook kwenye ukurasa wa waliosoma Kisutu na Kisutu Primary School.
Kwa upande wa K-Mondo, Mangustino alisema watatambulisha pia mtindo wao mpya wa kiuno na bega huku pia wakimtambulisha pia mpiga gitaa la rythim Victor Victory pamoja na mpiga besi aliyerejea tena kwenye bendi hiyo Joshua Bass.
K-Mondo Ijumaa hii itatumbuiza kwenye ukumbi wake wa nyumbani wa Triz Motel, Mbezi Beach wakati Jumamosi watakuwa Green Palm Resort Kunduchi.

Comments