WAVU YAKUNWA NA VIPAJI UMMISETA

CHAMA cha mpira wa wavu nchini (TAVA) kimeridhishwa na kiwango cha mchezo huo kinachoonyeshwa na wachezaji chipukizi kupitia michezo ya shule za sekondari nchini (UMMISETA) inayoendelea katika hatua ya kanda kote nchini.
Katibu Msaidizi wa TAVA, George John alisema jana kuwa chama chake kimetuma timu ya wataalamu wa mchezo huo kufuatia hatua mbalimbali za michuano hiyo ili kubaini vipaji vilivyopo kwa lengo la kuviendeleza.
Alisema zoezi hilo linaendelea vizuri kiasi cha kutosheleza kutoa dira ya maendeleo endelevu ya mchezo huo uliopoteza umaarufu wake katika miaka ya karibuni hasa baada ya michezo ya mashuleni kusimamishwa na serikali ya awamu ya tatu.
"Tumepata mwelekeo sahihi na sasa tunaweza kuandaa timu za taifa za vijana, jambo ambalo katika miaka miwili iliyopita lilikuwa ni ndoto," alisema.
Alisema uwekezaji kwa chipukizi ndio msingi pekee imara kwa mchezo wa mpira wa wavu kama ambavyo nchi majirani za Kenya na Uganda, zimekuwa zikifanya.
John alisema kwa muda mrefu sasa mpira wa wavu umekuwa ukichezwa majeshini pekee kutokana na kukosa msisimko mashuleni jambo ambalo sasa limepata tiba.
Aidha, aliipongeza serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kwa kusimamia urejeshwaji wa michezo mashuleni jambo litakalokuza michezo mingi midogo ambayo huendana na taaluma.
"Ilikuwa ni vigumu kugawa mipira ya wavu mitaani vijana wakacheza kirahisi kwani walio wengi hawaujui mchezo huu na mingine mingi ambayo msisimko wake huanzia mashuleni," alisema.

Comments