WASAMBAZAJI WADAIWA KUDIDIMIZA VIPAJI VYA WASANII NCHINI

Wasambazaji wa kazi za sanaa nchini wametajwa kuwa chanzo cha kudidimia kwa vipaji vya wasanii nchini kutokana na kuendekeza faida katika kuuza kazi za wasanii pasipo kuzingatia maudhui na ubora wa kazi zao.

Hayo yamesemwa wiki hii na msanii pia mtafiti wa masuala ya sanaa nchini Innocent Nganyagwa wakati akizungumza na wadau wa sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu ndani ya Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Alisema kwamba,wasambazaji wa kazi za sanaa wamekuwa wakijikita kwenye kuwaahidi wasaniii fedha na magari ili watoe albam au kazi za sanaa bila kuzingatia ubora na maudhui hali ambayo imekuwaikisababisha kazi hizo zikose ubora na maadili ndani yake.

“Zamani wakati sanaa ni ridhaa,kazi za sanaa zilikuwa na weledi na zenye tungo zilizotukuka ndani yake lakini siku hizi weledi umepotea,wasanii wakishaahidiwa gari na milioni tatu na wafanyabiashara basi atalipua kazi haraka ili iingie sokoni.Hapa tutapata tungo bora?” Alihoji Nganyagwa.
Aliongeza kwamba,uwepo wa nyimbo za taifa na uzalendo vilisaidia sana upatikanaji wa tungo za sanaa zilizotukuka na halisi tofauti na sasa ambapo wasanii wamekuwa ni wa kuiga kila kitu pasipo kuzingatia uhalisia wa mazingira kutokana msukumo wa fedha.
“Kadri siku zinavyosonga mbele,wasanii wamekuwa wakitanguliza fedha kuliko uhalisia na maisha ya jamii inayowazunguka.Fedha zimekuwa mbele uhalisia nyuma.Hili ombwe katika sanaa ndilo limekaribisha mamluki katika sanaa kwa sababu kilichoko mbele ni fedha na si tungo na ubora katika sanaa” Aliongeza Nganyagwa.
Mbali na wasambazaji,uhaba wa miundombinu kwa wasanii,kubadilishwa matumizi kwa kumbi mbalimbali za burudani na kukosekana kwa sheria na sera madhubuti ya sanaa vilitajwa kama moja ya sababu ya kukosekana kwa tungo bora na madhubuti kwa wasanii.
Alihitimisha kwa kutoa wito kwa wasanii kuzingatia weledi katika kazi za sanaa na kuhakikisha wanatafuta msaada huo kila inapobidi kwani wataalam wapo.Aliwataka kuacha kufanya kazi za sanaa kwa kusukumwa na fedha bila kuzingatia uhalisia.

Comments