TFF, KWA KUMTELEKEZA MWASYIKA IPO SIKU WACHEZAJI WATAIKIMBIA STARS


KITENDO kilichofanywa na Shirikisho la soka Tanzania (TFF), cha kuacha kumtibu kwa makusudi mlinzi wa kushoto wa Yanga, Stephano Mwasyika aliyeumia wakati wa maandaalizi ya Taifa Stars iliyokuwa ikijiandaa kucheza mchezo wa kimataifa na Msumbiji ‘Mambaz’, hakifai.
Ni jambo lisiloingia akilini na linaloshangaza mno, kwa TFF ya leo inayoongozwa na vijana wanaojua baya na zuri walioahidi kuleta maendeleo ya kisoka, kumuacha mchezaji kama huyu akijiuguza kibubusa.
Mwasyika aliyeumia goti, siku chache kabla ya kwenda kuivaa Mambaz katika mchezo maalum wa ufunguzi wa uwanja mpya wa Taifa wa Msumbiji, aliishia kujiuguza biola uangalizi maalum wa uhakika kutoka TFF.
Kutokana na kujiuguza kwa staili hiyo, klabu ya Yanga ilishangaa kuona siku zikizidi kusonga bila ya mchezaji wao kupata ahueni na walipofuatilia walibaini kuwa goti hilo linahitaji kuepelekwa kwa wataalamu wa matatizo hayo waliopo nchini India.
Kwa mujibu wa Yanga waliwafahamisha TFF juu ya haja ya kumpeleka mchezaji huyo India ili akafanyiwe upasuaji wa goti hilo, lakini TFF ikawa ikipiga danadana suala hilo hadi Yanga ilipoamua kubeba msalaba huo.
Baada ya kusikia Yanga imeamua kumtibu mchezaji wake huyo, TFF eti ikaficha aibu kwa kuchangia shilingi 600,000 kwa ajili ya matibabu hayo, ambayo Yanga wanadai kuwa pamoja na tiketi yatagharimu karibu shilingi milioni nane kwa kuwa gharama za matibabu pekee ni shilingi milioni saba.
Ni jambo la kusikitisha sana, linalohuzunisha na kuudhi, nilitegemea TFF, ingebeba  mzigo huo kwa sababu ni wajibu wake kubeba dhamana ya wachezaji wanaoitumikia timu hiyo.
Ni TFF hii hii iliyotutangazia hivi majuzi kuwa inapanga kuishitaki kwa Shirikisho la soka la kimataifa (FIFA), klabu ya Đồng Tâm Long An ya Vietnam, kwa sababu ya kuwazuia wachezaji wake Danny Mrwanda na Abdi Kassim ‘Babi’, wasijiunge na Taifa Stars.
Klabu hiyo iliwazuia wachezaji hao wakati Stars ikijiandaa kuikabili, Jamhuri ya Afrika ya Kati mchezo uliopigwa huko Bangui, wiki iliyopita na Stars kuchapwa mabao 2-1.
Hivi kama TFF hii ndiyo inawatekeleza wachezaji kwa staili hii, ni klabu gani itakayokuwa tayari kuwaachia wachezaji wake waje kuumia na kutekezwa ghalafu yenyewe iingie katika tabu ya kuwatibu?.
Gharama hizi za matibabu ni mzigo kwa klabu, TFF wanao wadhamini na siku zote wamekuwa wakizipigia kelele klabu kuhakikisha zinawakatia bima wachezaji wake, leo inakuwaje wao washindwe kumtibu mchezaji kwa bima?.
Hapana huu ni utani unaokera usiokubalika kabisa, TFF wanapaswa kuwatibu wachezaji wake wote watakaoumia wakati wa mazoezi au mechi za Taifa Stars, timu za vijana na timu ya wanawake ‘Twiga Stars’.
Leo Yanga wanamtibu Mwasika, kwa sababu wanawaonea aibu viongozi wa TFF, lakini kesho ataumia mchezaji kutoka kwenye hizo timu za nje ambazo TFF wanataka kuzishitaki FIFA kwa kuwazuia wachezaji, tunadhani itakuwa vipi?
TFF inapaswa kufahamu kuwa, katika ulimwengu wa soka la sasa hakuna sababu ya kushindwa kumtibu mchezaji kwa namna yoyote ile, kwa sababu tiba kwa wanamichezo zipo ijapokuwa baadhi ya tiba hizo zinahitaji gharama kubwa, kama hizi za kuwapeleka wachezaji kutibiwa nje ya nchi.
Iwapo TFF wataendelea na mtindo huu nachelea siku chache zijazo klabu zitawazuia wachezaji wake na hili la Mwasika linaweza kutumiwa kama ushahidi na kielezo cha utetezi wa timu dhidi ya TFF mbele ya vyombo vya kutoa haki katika medali ya michezo.
TFF isidhani kuwa klabu zitaendeela kuwa kondoo wa kukubali kufanywa na kuburuzwa kwa staili hii, kuna siku watagoma na watakapogoma Shirikisho hilo litakuwa katika wakati mgumu.
Hii ni kutokana na kwamba TFF inazitegemea klabu kwa ajili ya kuwapata wachezaji wa kuunda vikosi vyake mbali mbali, lakini ni klabu gani itakayokuwa tayari kubebeshwa gharama kubwa namna hii za matibabu bila sababu za kimsingi?.
Ni miaka ya hivi karibuni tu ambapo wachezaji wameanza kukubali kuichezea Stars kwa moyo wao wate na hii ni baada ya nahodha wa zamani wa Stars, Leodegar Tenga, kutwaa uongozi wa Shirikisho hilo lakini hili linalotokea sasa litawakimbiza tena.
Sidhani kama Mwasika atakuwa tayari tena kuichezea Stars, wakati anajua kuwa akiumia itabidi faimilia yake imtibie ama viongozi wake waingiwe na huruma kama ilivyokuwa safari hii vinginevyo atadumu na ulemavu.
Lakini hilo sio kwa Mwasika pekee, bali wachezaji wote wanaoona kile alichofanyiwa mwenzao itabidi wajiulize mara mbili mbili kama wakubali mwito wa kuitumikia Stars ama laa.

Comments