TAARIFA MBALIMBALI TOKA TFF

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAREHE 14 JUNI 2011
UFAFANUZI KUHUSU UCHAGUZI WA VILLA SQUAD FOOTBALL CLUB (VILLA) NA CHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF

1.                   UTANGULIZI.

            Hivi karibuni kumekuwa na maelezo mbalimbali katika vyombo vya
habari kuhusu uchaguzi wa Klabu ya Villa na wanachama wengine wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). TFF inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao kuhusu
uchaguzi huo na chaguzi nyingine za wanachama wa TFF.

            Kila mwombaji uanachama wa TFF hana budi kutimiza masharti
yalivyoainishwa kwenye Katiba ya TFF ili kuwa mwanachama wa TFF. Kati ya
masharti  hayo ni Tamko la kimaandishi kuwa anakubali kufuata Katiba ya TFF,
Kanuni na maagizo katika muundo wake wa sasa na mabadiliko ya baadae na maamuzi
ya FIFA, CAF, CECAFA, TFF na vyombo vyake (Ibara ya 7(2)(c) na Tamko kwamba
atahakikisha kwamba Katiba ya TFF inaheshimiwa na wanachama wake na mtu yeyote
mwenye mahusiano naye (Ibara ya  7(2) (d).

            Baada ya kutimiza masharti yote ya maombi ya  kuwa mwanachama, kila
mwanachama wa TFF anawajibika, pamoja na kutimiza masharti na matakwa mengine ya
kikatiba:

            Kuwa mwaminifu na mtiifu kwa TFF kwa maana ya kutofanya vitendo
vinavyokwenda kinyume na matakwa ya TFF kama ilivyoanishwa kwenye Ibara ya 12
(1) (b).

            Kufuata Katiba,  kanuni, maagizo na maamuzi ya FIFA, CAF, CECAFA na
TFF. (Ibara ya12 (1) (d)).
 Kutokuwa na uhusiano wowote wa kimichezo na wanachama waliosimamishwa au kufukuzwa. (Ibara ya12 (1) (k)). 
Kutimiza wajibu wowote unaotokana na Katiba, Kanuni, maagizo na
maamuzi ya TFF. (Ibara ya12 (1) (n)).

            Kutopeleka masuala ya mpira wa miguu katika mahakama ya kawaida ya
Sheria. (Ibara ya12 (2) (e)).

            Mamlaka ya kusimamia uchaguzi wa viongozi wa  TFF na  wa wanachama 
wote wa TFF yamekasimiwa kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa mujibu wa Katiba ya
TFF Ibara ya 49 (1).

            Kanuni za Uchaguzi za TFF na wanachama wake zimetungwa na
kuidhinishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya
34(k).

 2.  MCHAKATO WA UCHAGUZI WA VILLA SQUAD FOOTBALL CLUB
Klabu ya Villa ni mwanachama wa TFF kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 5 (3) na 6(5).
Katiba ya Villa Ibara ya 1 (6) inatambua Mamlaka ya TFF. Ibara hiyo
inasomeka hivi:   “Klabu ya mpira wa miguu ya Villa Squad ni mwanachama wa TFF,
itaheshimu katiba, kanuni, maagizo na maamuzi ya TFF na kuhakikisha kuwa
zinaheshimiwa na wanachama wake”.
Pamoja na matakwa hayo hapo juu, Katiba ya Villa katika kuzingatia
uanachama wa Villa kwa TFF inazingatia pamoja na matakwa mengine haya yafuatayo
kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Villa:

            Ibara ya 11: Wajibu wa wanachama wa Villa; Kila mwanachama wa Klabu
ya Mpira wa miguu ya Villa Squad atakuwa na wajibu ufuatao zaidi ya ule
uliotajwa kwenye Kanuni za Asasi:


Ibara ya 11 (1) (c): Kukubali kufuata Katiba hii,  kanuni, maagizo na maamuzi ya
Klabu ya miguu ya Villa Squad na TFF.

(Ibara ya 11 (2) (b)): Kutopeleka masuala ya mpira wa miguu katika mahakama ya
kawaida ya Sheria.


            Ibara ya 25:Mtu yeyote anayegombea nafasi yoyote ya Klabu ya mpira
wa miguu ya Villa Squad hana budi kutimiza masharti yafuatayo:

1.   Awe na uzoefu wa uendeshaji mpira wa miguu uliothibitishwa.
2.   Asiwe na hatia yoyote ya kosa la jinai na kuhukumiwa kifungo bila ya kupewa
uchaguzi wa kulipa faini.
3.   Awe na umri angalau kuanzia miaka 18.
4.   Awe anajua kusoma na kuandika na awe na elimu ya msingi hadi sekondari.
5.   Awe na cheti cha elimu ya msingi na sekondari.

            Katiba ya Villa, kama zilivyo katiba za wanachama wa TFF inatambua
mamlaka ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF. Ibara ya 40(5) ya  Katiba ya Villa
inasomeka: Kamati hii itafanya kazi chini ya kamati ya uchaguzi ya TFF.

            Kwa kuzingatia wajibu wake wa kikatiba kama ilivyoainishwa hapo juu,
TFF iliiagiza Klabu ya Villa kuanza mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Klabu ya
Villa kuanzai tarehe 02 Mei 2011 kwa barua  yenye Kumbukumbu Na.
TFF/ADM/EC11./09 ya tarehe 30 Aprili 2011 na pia kuagiza kuwa uchaguzi huo
ufanyike kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na ukamilike
kabla ya tarehe 20 Juni 2011.
:
            Baada ya Kamati ya Uchaguzi ya Villa kukamilisha zoezi la usaili, 
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa barua yenye kumbukumbu Na. TFF/ADM/EC.11/17 ya 
tarehe 06 Juni 2011 iliiomba Kamati ya Uchaguzi ya Villa kuwasilisha taarifa ya
mchakato wa uchaguzi, ikitimiza majukumu yake ya kikatiba na kikanuni ya
kutathmini na kusimamia uchaguzi wa wanachama wa TFF.

            Baada ya kupata taarifa kutoka Kamati ya Uchaguzi ya Villa, Kamati
ya Uchaguzi ya TFF ilifanya kikao na Kamati ya Uchaguzi ya Villa katika makao
makuu ya Klabu ya Villa hapo tarehe 08 Juni 2011, ili kupata ufafanuzi wa kina
kuhusu uzingatiaji wa Kanuni za Uchaguzi na kujadili matayarisho ya uchaguzi ili
kuhakikisha kama mahitaji yote ya kufanikisha uchaguzi uliokuwa umepangwa
kufanyika tarehe 12 Juni 2011 yamekamilika.

            Kwa kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF haikuridhika na maelezo
yaliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi ya Villa kuhusu matokeo ya usaili wa wagombea
na vielelezo vilivyotajwa na Kamati Uchaguzi ya Villa kuwapitisha baadhi ya
wagombea uongozi, Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa barua yenye kumbukumbu Na.
TFF/ADM/EC.11/18 ya  tarehe 09 Juni 2011 iliiagiza Kamati ya Uchaguzi ya Villa
uwasilishe TFF nakala  za fomu za kuomba uongozi za waombaji uongozi wote
waliopitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya Villa, zikiwa zimeambatanishwa na nakala
za uthibitisho wa sifa za wagombea uongozi, kwa mujibu wa Ibara ya 10 ya Kanuni
za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliagiza kufanyika
hivyo kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 26 (2)
inayoipa mamlaka Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuingilia mchakato wa uchaguzi wa
wanachama wa TFF wakati wowote ule kuangalia na kuthibitisha usahihi wa mchakato, kuhakiki na kujiridhisha kwamba Kanuni za Uchaguzi, matakwa ya Katiba
ya mwanachama wa TFF, Katiba ya TFF na FIFA  yanazingatiwa. 
Kamati ya Uchaguzi ya TFF, katika kikao chake kilichofanyika tarehe
10 Juni 2011 kupitia fomu za maelezo  ya wagombea uongozi wa Klabu ya Villa na
nyaraka za uthibitisho wa sifa za wagombea uongozi, ilibaini kuwa   wagombeaBw.
Mohamed Kea Mohamed, Bw. Ramadhani Soud Iddi, Bw. Alwan Mohamed Geyash, Bw. Ali
Mohamed Daddy Baucha, Bw. Ally Ahamed Mpemba Bw. Said Yusuf Chacha,  Bw. Idd
Mohamed Mbonde  na Bw. Abdalla D. Majurah hawakidhi  sifa za wagombea uongozi kama zilivyoainishwa kwenye ibara ya 25 (5) ya Katiba ya Klabu ya Villa.
Kwa kutotimiza masharti na sifa za uongozi kwa mujibu wa Katiba ya Villa, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaondoa katika orodha ya wagombea uongozi kwa nafasi walizoomba kugombea. Kamati ya Uchaguzi ya Villa ilitaarifiwa maamuzi hayo ya Kamati na kuagiza uchaguzi wa Klabu ya Villa Squad utafanyika kama ulivyopangwa tarehe 12 Juni 2011, kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya
Utendaji na kwamba  nafasi ya Mwenyekiti haina mgombea na itajazwa baadaye kwa mujibu wa Katiba ya Klabu ya Villa Squad Ibara ya 28(c), yaani kwenye uchaguzi mdogo wakati wa mkutano mkuu wa mwaka uonaofuata baada ya uchaguzi.
Kamati ya
Uchaguzi ya Villa ilitakiwa kwa barua ya TFF yenye kumbukumbu EC/TFF/06/2011/002
ya 10 Juni 2011kutekeleza maamuzi hayo ya TFF.
3.KUTOFANYIKA UCHAGUZI WA VILLA
 Kutofanyika kwa uchaguzi wa Villa ni ukiukwaji wa maagizo na maamuzi
ya TFF na ukiukwaji wa Katiba ya Villa na TFF.
Kuahirisha uchaguzi wa Villa kulikofanywa na mkutano mkuu wa Villa ni kukiuka Kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 10 (6) inayokataza kubadili tarehe ya uchaguzi au kufuta uchaguzi ambao umekwisha tangazwa na Kamati ya Uchaguzi bila idhini ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
 Kutoiruhusu Kamati ya Uchaguzi ya TFF ni kukiuka matakwa ya Katiba ya TFF Ibara ya 49(1) inayoipa mamlaka Kamati ya Uchaguzi ya TFF kusimamia chaguzi za wanachama wa TFF.

4.KUBADILI KATIBA BILA IDHINI YA TFF
  Kitendo cha kubadili Katiba ya Villa katika mkutano mkuu wa uchaguzi
ni kukiuka Katiba ya TFF Ibara ya 12 (1)(b) na (c).
 Kubadili vifungu vya Katiba ya Villa na kuweka vipengele vinavokinzana na Katiba ya TFF ni kukiuka Kanuni za Uchaguzi Ibara ya 6(a) na (b) na Katiba ya TFF ya 12 (1) (d) na (e).
Mabadiliko ya Katiba ya Villa yaliyofanywa na tarehe 12 Juni 2011 hayatatambulika na TFF.

5.KUFANYIKA KWA UCHAGUZI WA VILLA ULIOAHIRISHWA KIMAKOSA.
 TFF inaiagiza Kamati ya Uchaguzi ya Villa na uongozi wa Villa kutoendelea na vitendo vya ukiukwaji wa Kanuni za uchaguzi.
TFF inaiagiza Kamati ya Uchaguzi ya Villa na uongozi wa Villa kutekeleza maagizo na maamuzi ya TFF mapema iwezekanavyo kwa kukamilisha mchakato wa uchaguzi kama ilivyoelekezwa na TFF.
TFF inaiagiza Kamati ya Uchaguzi ya Villa na uongozi wa Villa kuhakikisha kuwa inakamilisha mchakato wa uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na kupata viongozi kabla ya Kikao kijacho cha Kamati ya mashindano ya TFF ambacho kitafanya maamuzi stahiki ya ushiriki wa Klabu ya Villa katika Ligi kuu, endapo Klabu ya Villa haitatekeleza majukmu yake ya kikatiba kwa taratibu zilizowekwa na TFF.
Kamati ya Uchaguzi ya Villa na uongozi wa Villa wanaagizwa kutekeleza maagizo hayo hapo juu ili kuepuka hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi wao na Klabu ya Villa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za TFF na Katiba ya  TFF, CECAFA, CAF na FIFA, endapo hawatatekeleza maamuzi ya TFF.
6. UCHAGUZI WA VIONGOZI WA WANACHAMA WA TFF
 TFF inasisitiza kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF itaendelea na majukumu yake ya kusimamia chaguzi za wanachama wa TFF na inawataka wanachama wote wa TFF kuendelea kuzingatia Katiba (zinazoendana na Katiba ya TFF) na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na za TFF katika michakato ya uchaguzi wa
viongozi wao.
Angetile Osiah
KATIBU MKUU

Comments