ONYESHO LA FASHION 4 VISION LAINGIZA MILION 15

 Meneja Masoko wa Benki ya Exim Tanzania Linda Chiza(kushoto) akipeana mkono na
Rais wa Lions Club Tanzania Frank Goyayi wakati wa makabidhiano ya mfano wa
hundi ya milioni moja kutoka benki hiyo kuchangia matibabu ya wagonjwa wa macho
nchini.Katikati ni Mama Salma Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi na wa pili kushoto
ni Meneja Mkuu wa Benki ya Exim dinesh Arora na kulia ni Mkurugenzi wa benki
hiyo Hanif Jaffer.
Baadhi ya Wanamitindo walioshiriki katika onyesho maalumu la mavazi la ‘Fashion
4 Vision’ lililofanyika mwishoni mwa wiki Dar es Salaam maalumu kwa kuchangisha
fedha kwa ajili ya wagonjwa wa macho nchini ambapo sh. milioni 15/-
zilipatikana. Onyesho hilo lililoandaliwa na Lions Club kwa pamoja na Wabunifu
wa Mavazi Mustapha Hassanali na Jamila Veraswai na kudhaminiwa na Benki ya Exim
Tanzania.

ONYESHO  maalumu la mavazi llinalobeba ujumbe wa ‘Fashion 4 Vision’
lililofanyika mwishoni mwa wiki Dar es Salaam limechangisha sh. mil 15/-
zitakazosaidia matibabu ya wagonjwa wa macho nchini.
Onyesho hilo liliandaliwa na Lions Club Tanzania chini ya uratibu wa Wabunifu wa Mavazi Mustapha Hassanali na Jamila Veraswai na kudhaminiwa na Benki ya Exim
Tanzania ambapo vitu mbalimbali yakiwemo mavazi ya mitindo tofauti yalinadiwa na mgeni rasmi Mama Salma Kikwete kwa waliohudhuria.
Akizungumzia onyesho hilo Mama Salma aliipongeza Lions Club pamoja na wabunifu
Hassanali na Veraswai kwa kuwa na mawazo chanya ya kusaidia jamii ya kitanzania
ambapo pia aliwashukuru na kuwapongeza wote waliojitokeza katika onyesho hilo na

kuchangia kutunisha mfuko kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa husika.
“Ni mawazo yanayopaswa kuungwa mkono na mimi binafsi nawapongeza Lions pamoja na

wabunifu wetu kwa kuonyesha moyo wa imani kwa wenzetu wanaosumbuliwa na maradhi
lakini niwapongeze pia waliojitokeza leo na kuchangia fedha”,alisema Mama
Kikwete.
Kwa upande wake  Meneja Mkuu wa Benki ya Exim Dinesh Arora alisema pamoja na
udhamini wamechangia sh.milioni moja katika mfuko huo na kwamba hiyo ni katika
utekelezaji wa majukumu ya kawaida ya kibenki kwa jamii ya kitanzania
wanaochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa benki hiyo.
“Tumekuwa tunafanya biashara ya kibenki kama jukumu letu kuu lakini pia
tumekuwa na majukumu mengine kwa jamii inayotuzunguka hivyo udhamini pamoja na
mchango wetu katika hafla ya leo ni miongoni mwa utekelezaji wa majukumu hayo,”
alisema Arora.
Rais wa Lions Club Frank Goyayi alisema hafla hiyo ilitarajiwa kukusanya sh.
milioni 10/= lakini ni jambo la kutia moyo kuona wamevuka lengo na kwamba hiyo
inawahakikishia kuwa watafanikiwa katika yale waliyoyalenga kwa wagonjwa wa
macho nchini.
“Tumefarijika na kututia moyo kwa kiasi kikubwa na sasa tuna imani ya kufanikiwa katika yale tuliyoyalenga,tunawashukuru wote waliojitolea kudhamiani na
kuchangia kwa moyo wao wa upendo kwa wenzao wanaosumbuliwa na maradhi,” alisema
Goyayi.

Comments