MAGORI AWEKWA KITI MOTO NA BARAZA LA MAADILI



ALIYEKUWA Makamu wa kwanza wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Crecencius Magori, jana aliburuzwa mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi na Watumishi wa Umma, kwa kushindwa kujaza fomu za kutangaza mali na madeni kwa mujibu wa sheria.
Magori, ambaye ni Mkurugenzi wa Matekelezo wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), akijitetea mbele ya Baraza hilo, chini ya Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Damiani Lubuva, alisema kuwa, alikuwa hajui kama ana wajibu wa kujaza fomu hizo kwa mujibu wa sheria.
“Mimi toka nilipokuwa Mkurugenzi mwaka 2005, sijawahi kujaza fomu wala sizijui na nimesikia katika vyombo vya habari kuwa, nami ni mmoja ya washtakiwa ambao sijajaza fomu za kutangaza mali na madeni kwa mujibu wa sheria, ila kuanzia sasa nitakuwa nazifuata mwenyewe kabla sijaletewa ofisini,” alisema Magori.
Hata hivyo, Magori ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Masoko na Habari ya TFF, aliomba radhi mbele ya baraza hilo na kueleza kuwa, hakuwa na sababu ya kutofanya hivyo, kwa kuwa hana mali za kutisha na anaishi maisha ya kawaida kama ilivyo Watanzania wa kawaida.
Magori, ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati mbalimbali za klabu ya Simba yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam, alisema mbali na hatua hiyo lakini amejifunza kutokana na hatua ya kufikishwa mbele ya baraza hilo, hivyo atahakikisha anaweka mambo yake sawa ili kumaliza tatizo hilo la kisheria.
Alisema tangu alipoanza kazi hajawahi kuziona fomu hizo zaidi ya kusikia kuwa kuna fomu za kutangaza mali ambapo alihisi ni kwa vingozi wa kisiasa hasa wabunge  na madiwani pekee.
Hata hivyo, maelezo hayo ya utetezi yaliwafanya wanasheria wa Sekreterieti ya Maaadili ya Viongozi wa Umma kuwa na kazi nyepesi na hata kukosa maswali mengi kwa Magori, huku wakisisitiza na kuliomba Baraza hilo kumchukulia hatua za kisheria kama mtumishi wa umma.
Baraza hilo limemaliza vikao vyake vya kusikiliza mashauri hayo na kuahirisha shauri namba 51/2011 Mathias Mgata, ambaye ni diwani wa Kata ya Kanazi mkoani Kigoma kutokana na vielelezo vilivyotolewa kutosomeka vizuri.

Comments