KONGO WAPETA KOMBE LA DUNIA U-17

PACHUCA, Mexico

WAWAKILISHI wa Afrika, Congo wamefanikiwa kufuzu kwa hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia la Fifa U-17 baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 na Korea Kaskazini, huku Rwanda wakiagaa fainali hizo.
Matokeo hayo yanaifanya Congo kumaliza ya pili kwenye Kundi A nyuma ya Mexico na sasa watacheza na kati ya Uruguay au England kwenye mtoano.
Christ Nkounkou aliifungia Congo bao la kusawazisha baada ya Ju Jong Chol kuifungia Korea bao la kuongoza dakika ya 14 ya mchezo.
Nkounkou alikuwa mwiba wakati wote kwa ngome ya Wakorea hao lakini mashuti yake mengi yalikumbana na kizuizi cha kipa aliyekuwa makini kuokoa hatari zote.
Wakati huo huo; Si Rwanda wala Canada aliyeweza kusonga mbele kwenye michuano hiyo pamoja na timu hizo kumaliza kwa suluhu katika mchezo uliokuwa na upinzani mkubwa uliofanyika Uwanja wa Estadio Hidalgo.
Mchezo wa mwisho wa Kundi C ilishudia England ikimaliza kinara kwa pointi saba wakifutiwa na Uruguay kwenye mchezo uliofanyika huko mjini Pachuca.
Mchezo huo ulianza kwa taratibu huku kila timu ikijaribu kuwasoma wapinzani wake, lakini mshambuliaji wa Rwanda, Andrew Buteera mara mbili aliiwatoka mabeki wa Canada na kupiga shuti lililopanguliwa na kipa Quillan Roberts na jingine liligonga mwamba na kutoka nje.

Comments