KOMBE LA NAHEKA KUFANYIKA MIKUMI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Diwani wa viti maalum wa Tarafa ya Mikumi wilaya ya Kilosa, Mariam Naheka anatarajia kuanzisha michuano ya soka kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa Kata nane zilizomo ndani ya tarafa ya Mikumi, Kilosa mkoa wa Morogoro.
Tayari maandalizi kwa mashindano hayo yameshaanza kwa diwani Naheka kugawa mipira 55 kwa shule zilizomo kwenye tarafa hiyo ambazo ni Kata za Mikumi, Kidodi, Ruaha, Vidunda, Ruhembe, Kisanga, Uleling'ombe na Malolo.
Nheka ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Chama cha Soka wilaya ya Kilosa, ameamua kugawa mipira hiyo mashuleni baada ya kubaini kuwa shule nyingi hazina mipira ya kufanyia mazoezi.
Ingawa hakuwa wazi kuweka tarehe rasmi ya kuanza kwa mashindano hayo, Naheka amezitaka shule zote zitakazopewa/zilizopewa mipira hiyo kuanza mara moja mazoezi ya kujiweka fiti.
Alisema kuwa michuano hiyo ya Naheka Cup itaanza kwa shule kwa shule zilizomo kwenye kata moja kuchuana na kupatikana kwa bingwa wake ambaye ataiwakilisha Kata hiyo kwenye ngazi ya Tarafa.
Kwa sasa Naheka alisema kuwa anasubiri kukaa na walimu wakuu wa shule husika ili wapange ni zawadi gani ambazo zitatolewa kwa mabingwa wa Kata na wa Tarafa.
Lakini aliahidi zitakuwa nzuri na kila bingwa anaifurahia kuipata.
Akizungumzia malengo ya mashindano hayo, Naheka ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha soka la wanawake mkoa wa Morogoro, alisema yana nia ya kuibua vipaji kuanzia kwenye ngazi za chini.
Kutafuta wachezaji bora ambao baadaye wakiendelezwa wanaweza kuwa hazina kubwa kwa taifa.
Lakini pia, watoto watapata fursa ya kufahamiana, kufurahia michezo na kujenga udugu miongoni mwao hivyo akaomba wadau wengine kujitokeza katika kuendeleza soka kwa vijana.
Mariam Naheka ni mke wa Mkurugenzi wa Fedha wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Ni Diwani Viti maalum (CCM), Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Kilosa, Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake mkoa wa Morogoro.

Comments