Cassim aahidi makubwa usiku wa mahaba


.Matonya, Khanga Moja Ndembe Ndembe ndani

NA MWANDISHI WETU
MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Kassim Mganga ‘Cassim’, ameahidi kufanya shoo bab kubwa katika onyesho lililopewa jina la Usiku wa Mahaba, litakalofanyika Club Billicanas, Dar es Salaam, Jumapili hii.

Shoo hiyo ya aina yake, itasindikizwa na burudani kadhaa za ukweli hapa nchini, zikimhusisha msanii wa Bongo Fleva, Seif Shaaban ‘Matonya’ na kundi maarufu la unenguaji la Khanga Moja Ndembe Ndembe.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Kassim alisema kuwa onyesho hilo ni maalum kwa ajili ya utambulisho wa video yake mpya inayokwenda kwa jina la ‘Tajiri wa Mahaba’ pamoja na utambulisho wa kampuni yake iitwayo, Manza Bay
Entertainment.

Alisema kuwa baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu, ameamua kuibuka upya, akiapa kuwapa wapenzi wa burudani kile kitu roho inapenda ili kukata kiu yao katika upande wa burudani.

“Nimekuwa kimya kwa muda mrefu nikitafakari ni vipi ninaweza kutoka upya na kukidhi matakwa ya wapenzi wa burudani nchini na nje ya Tanzania,” alisema Kassim ambaye ni mkali wa nyimbo za kubembeleza.

Msanii huyo aliongeza: “Kwa sasa Kassim amezaliwa upya, mashabiki wangu na wa burudani waje kwa wingi Club Billicanas kupata burudani ya hali ya juu, zaidi ikiwa ni kushuhudia ujio mpya wa Kassim pamoja na Matonya.”

Alisema kuwa kama ilivyo kwake, Matonya naye alikuwa kimya kwa muda wa miaka miwili ambapo siku hiyo naye atatambulisha wimbo wake mpya unaoitwa ‘Utakula Ulipopeleka Mboga’ kabla ya Khanga Moja Ndembe Ndembe ‘Laki Si Pesa Milioni Uadui’, kufunga kazi.

Alizitaja baadhi ya nyimbo zitakazochezwa siku hiyo kuwa ni zile alizoimba yeye kama Awena, Amore na Haiwezekani, wakati Matonya atapagawisha na vibao vyake vya Anita, Spare Tyre, Taxi Bubu na nyinginezo.

Onyesho hilo linalotarajiwa kuvuta hisia za wapenzi lukuki wa burudani nchini, limedhaminiwa na kituo cha televisheni na redio cha Clouds FM.

Comments