HOTUBA FUPI YA MKURUGENZI MTENDAJI WA BENKI YA AZANIA,CHARLES SINGILI KATIKA HAFLA YA KUTOA FEDHA KWA MFUKO WA SICKLE CELL

Mabibi na Mabwana,Kila siku mpya ni fursa nzuri ya kutumika, kikazi na kijamii, nami nafurahi kuwa asubuhi ya leo ni nzuri kwa kuwa tunatumika kijamii kama Benki kwa upande wa jitihada za kudhibiti au kueneza habari kuhusu ugonjwa wa sickle cell
Ndugu Waandishi wa Habari,Sickle cell tunaita ugonjwa kwa kukosa neno zuri zaidi la Kiswahili, ni hali ambayo hurithiwa ambayo husababisha seli nyekundu za damu kuwa kama herufi c kutokana na hitilafu ya vinasaba na hivyo kuathiri uwezo wa seli hizo kubeba damu ama husababisha shida kwa kuziba mirija midogo ya damu. Ni tatizo ambalo husababisha kufeli kwa viungo muhimu linapojitokeza kwa kuzuia upatikanaji wa oksijeni kwenye viungo hivyo na kama hakujapatikana huduma ya haraka watu walio na tatizo hili hupata maumivu makali na mara nyingine hufa mapema.
Sickle cell anemia huleta maumivu ya muda mrefu kwa baadhi ya watu na kwa mujibu wa takwimu, tatizo hili huathiri zaidi watu wenye asili ya Africa hasa walio kusini kwa jangwa la sahara. Watoto takriban 15,000 huzaliwa na shida hii hapa Tanzania kila mwaka na kati ya asilimia 50 hadi 80 ya watoto hawa hufa kabla ya kufikisha miaka 5.
Takwimu hizi pia zinasema kwamba Tanzania imeshika nafasi ya nne duniani kwa kuwa na kesi nyingi zilizoripotiwa za ugonjwa huu.
Ndugu Waandishi wa Habari
Kama nilivyosema awali, tatizo la sickle cell ni la kurithi na hutokea pale ambapo watu wawili wenye damu zenye tabia/uwezekano kimuundo za sickle cell wanapo pata mtoto. Hii haimaanishi kuwa wazazi hao wana dalili au kutaabika kwa ugonjwa huu.
 Kwa minajili hiyo basi, sisi kama benki ya Azania tunaona namna mojawapo ya kudhibiti ugonjwa huu ni kwa uenezi wa taarifa zake na watu wanapotaka kuwa na watoto basi wapime damu zao kuona kama kuna uwezekano wa sickle cell kwao. Kitakwimu ugonjwa huu hupunguza urefu wa maisha, ambapo kwa wastani watu wenye hali hii huishi miaka 43 kwa wanaume na 48 kwa wanawake, japwapo wanaoishi zaidi ya wastani huu.
Tunaungana na jitihada za mashirika mengine na taasisi katika kuchangia jitihadaza kueneza habari za ugonjwa huu kwa kupitia mfuko huu wa sickle cell leo kwa kuchangia shilingi milioni tatu.
Tunaamini kwamba ufahamu ni chemchemi ya mabadiliko na kwa kupitia taarifa sahihi basi wale wanaoathirika na hali hii wataweza kufuata taratibu za kimatibabu ili kuongeza urefu wa maisha yao, pamoja na kupunguza maumivu yanayotokana na hali nyemelezi kama vile malaria, anemia na maambukiz bacteria za ugonjwa huu ambao hautibiki.

Comments