FEDHA ZA UBINGWA YANGA ZALIPIA DENI CECAFA

KLABU ya Yanga imekubali yaishe kwa kulipa faini ya dola 20, 000 za Marekani kwa Baraza la Vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), walizokuwa wakidaiwa kwa kosa la kuikacha Simba katika michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2008.
Awali, Yanga ililimwa faini ya dola 30,000 za Marekani na kutocheza michuano hiyo kwa miaka mitatu, lakini hivi karibuni klabu hiyo iliomba radhi na kutaka ipunguziwe faini na ndipo ikatakiwa kulipa kiasi hicho cha dola 20,000.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Angetile Ossiah alisema uamuzi wa sehemu ya fedha hizo kulipia deni, ni ombi la uongozi wa klabu ya Yanga.
Alisema, awali Shirikisho hilo lilitaka kuilipa klabu hiyo fedha zao za zawadi kwa awamu mbili, lakini Yanga wakagoma wakitaka kulipwa fedha zao zote kwa kigezo ili waweze kuzitumia kulingana na mahitaji yao.
Ossiah alisema wakati TFF wakitaka kutimiza matakwa ya klabu hiyo ya kulipwa fedha zote kwa pamoja, Yanga wakawasilisha ombi wakitaka sehemu ya fedha hizo zitumike kulipa deni la klabu hiyo kwa Cecafa.
Kiongozi huyo alisema sambamba na ombi hilo, Yanga walitaka kiasi kitakachosalia baada ya kutoa dola 20,000, ndicho kiende mikononi mwao ili wajivue kwenye kifungo cha Baraza hilo.

Comments