FABREGAS ASAINI MIAKA MIWILI YANGA,AKABIDHIWA JEZI NAMBA NANE



Na Dina Ismail
KIUNGO mpya wa Yanga Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ juzi amekabidhiwa jezi namba nane za klabu hiyo baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuwatumikia mabingwa hao.
Habari kutoka Yanga zinasema kwamba kiungo huyo wa kimataiga wa Rwanda mara atakapoanza kuitumikia timu hiyo atakuwa akitumia jezi hiyo iliyowahi kutumiwa na wachezaji nyota wa kihistoria wa Yanga kama Sunday Manara, Athunm Abdallah China na Salvatory Edward.
Hata hivyo, uwezekano wa Haruna kuanza kuichezea Yanga katika michuano ya Kagame utategemea makubaliano baina ya klabu yake mpya na ya zamani kwani mkataba wake na APR unaishia Septemba.
Mazungumza baina ya Yanga na APR yanaendelea ili nyota huyo aanzf kuitumikia katika Kagame itakayoanza kutimua vumbi jijini Dar es Salaam na Morogoro kesho ambapo Yanga itaanza kazi jumapili kwa kukipiga El Mereikh ya Sudan.
Mbali na Haruna nyota wa kigeni wengine waliosajiliwa Yanga ni Yaw Berko (GHANA), Tonny Ndolo (Uganda),Davis Mwape (Zambia) na Kenneth Assamoh wa Ghana.
Iwapo mazungumzo kati ya APR na Yanga yatashindikana kwa sasa Yanga itamsajili mshambuliaji chipukizi wa Uganda, Kiza Hamis ambaye tayari ameshaingia mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo.
Katika kombe la Kagame kikosi cha Yanga kitapambwa na nyota wapya wa nyumbani pia ambao ni makipa Shaban Kado, Said Mohammed, mabeki Oscar Joshua, Godfrey Taita, Julius Mrope, Pius KIsambale na Rashid Gumbo.
Yanga imewahi kutwaa kombe hilo mara tatu 1975 iliyopigwa Zanzibar, 1993 iliyopigwa Uganda na 1999 pia ilipigwa Uganda.

Comments