VICTOR COSTA ATAKA KUREJEA SIMBA SC

VICTOR Costa amethibitisha kuwa anarudi nyumbani Tanzania kujiunga na Simba kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Na amewapiga mkwara mabeki wa Simba kuwa atapambana nao kwani ana uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza ikiwa pamoja na kurejea katika kikosi cha Taifa Stars.
Costa ambaye ni beki wa zamani wa Simba alisema baada ya kuitumikia klabu ya HCB de Songo ya Msumbiji kwa miaka mitatu, sasa ni muda muafaka wa kurejea nyumbani na kuichezea klabu yake ya zamani.
"Nimezungumza na Simba, kila kitu kimekwenda sawa, narudi si kufanya majaribio, ila nakuja kucheza mpira.
"Kiwango changu si cha kufanya majaribio, ila ni cha kusajiliwa moja kwa moja na hilo halina tatizo kwani narudi wiki hii kuja kusajiliwa Simba," alisema Costa, maarufu kwa jina la Nyumba.
Costa alisema: "Hapa nalipwa vizuri, lakini nimezungumza na viongozi wa Simba tumekubaliana kuwa watanilipa vizuri, hivyo nakuja kuonyesha vitu vyangu kwani huku ilikuwa ngumu kuonekana kwa mashabiki wa Tanzania," alisema beki huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar.
"Uongozi wa klabu yangu umeniruhusu kuondoka, na wameniambia kuwa wakati wowote milango ipo wazi kama nikihitaji kurejea, nashukuru kwani kwa miaka mitatu tumeishi vizuri."
Juzi Jumapili, timu ya Costa ilicheza mchezo wa fainali na Shingale katika Kombe la Tasa na huo ndio ulikuwa mchezo wa mwisho kwa beki huyo wa zamani wa Taifa Stars.
"Wiki hii, nitakuwa Dar es Salaam na Jumatatu ijayo nitajiunga na Simba."
Hiyo ina maana kuwa Simba sasa itakuwa na mabeki sita wa kati wengine wakiwa ni Kelvin Yondani 'Vidic', Juma Nyosso, Obadia Mungusa, Shomari Kapombe, Derrick Walulya.

Comments