WAZIRI MKUU PINDA AHIMIZA UFANISI KATIKA MAENEO YA UWEKEZAJI


Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mizengo Pinda amesema ipo haja kwa waafrika kufanya jitihada za makusudi kuongeza ufanisi katika uzalishaji ili kuendena na ushindani wa mahitaji ya walaji katika soko la dunia na kwingineko katika mataifa yaliyoendelea.

Waziri Mkuu aliyasema hayo alipofungua Mkutano Mkuu wa Maeneo Huru ya Uwekezaji Afrika (AFZA) jana katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam jana ambao unaendelea kwa siku tatu hadi kesho chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia na EPZA Tanzania.

Alisema ili Waafrika wafanikiwe katika hilo,serikali za nchi husika hazina budi kutoa kipaumbele katika kuendeleza maeneo huru ya uwekezaji katika nchi zao kwani ndio nguzo muhimu ya maendeleo katika mataifa mengi ambayo tayari yameendelea.

“Ni fursa kubwa kwetu kama watanzania lakini kwa nchi za afrika kwa ujumla wake kwani mkutano huu utawawezesha kutoa mawazo chanya ya jinsi mtakavyoweza kuboresha ufanisi wa kiutendaji na uzalishaji katika maeneo huru ya uwekezaji katika maeneo yenu hivyo nachukua nafasi hii pia kuzihimiza serikali zetu ziweke mkazo katika mikakati ya uwekezaji”, alisema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa EPZA Tanzania Dkt Adelhelm Meru alisema mkutano huu pamoja na wengine unajumuisha wadau kutoka maeneo huru ya uwekezaji katika nchi tofauti za Afrika, watunga sera kutoka sekta za umma, wataalam kutoka Benki ya Dunia, Ulaya, Asia na Amerika. Meru aliongeza kwamba hii ni fursa kwa wawekezaji wa ndani kuona changamoto mbalimbali wanazozipata wawekezaji wengine na kutafuta njia ya kujinasua nazo.

Aliongeza kuwa mkutano pia utasaidia wawekezaji wa ndani kujenga mbinu mbalimbali za jinsi ya kuunda ukanda huu wa uwekezaji Afrika ili kuwawezesha wao  kwaa wawezeshaji wakuu katika kuhakikisha malengo ya maendeleo ya millenia
yanafikiwa.
“Mkutano huu utawasaidia wawekezaji wa kizalendo kuweza kutafuta njia za pamoja
ambazo zitasaidia kuendeleza maeneo huru ya uwekezaji ili kufikia malengo ya
millennia lakini pia ni fursa nzuri kwetu kama waaafrika kujifunza mbinu mbadala
za kuinuka kiuchumi kupitia maeneo haya ya uwekezaji”, alisema Meru.

Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Jukumu la Maeneo Huru ya Uwekezaji katika kufikia
malengo ya Milenia 2015” ambapo wazungumzaji wakuu watakuwa Waziri wa Viwanda na
Biashara, Dk Cyril Chami, Mwenyekiti wa AFZA Dk. N. Abe wa Nigeria, Mkurugenzi
Mkuu Mkazi wa Benki ya Dunia Afrika, John McIntire na Dk Meru kama mwenyewe.

Mada nyingine zitawasilishwa na Alberto Castronovo wa AFZA kutoka Italia,
Profesa Samuel Wangwe ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA Tanzania , Thomas
Farole kutoka Benki ya Dunia na wataalamu kutoka China, Jordan na Dubai ambako
maeneo ya uwekezaji yamepiga hatua kubwa.

AFZA ni shirika la kimataifa la hiari lililoanzishwa Oktoba 2004 Afrika Kusini
kwa lengo la kuendeleza ushindani katika maeneo huru ya uwekezaji ili kuendeleza
mageuzi ya kiuchumi barani Afrika.Mkutano mkuu wa kwanza wa AFZA ulifanyika


Abuja, Nigeria mwaka 2008 na huu utakuwa ni wa pili.

Comments