WADHAMINI WAMIMINIKA MISS MWANZA

HOTELI ya kitalii ya Gold Crest ya jijini hapa, imejitokeza kudhamini shindano la Miss Mwanza linalotarajiwa kufanyika Juni mwaka huu.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, msimamizi wa hoteli hiyo, Benny Mwangi, alisema kuwa hoteli hiyo imeamua kudhamini shindano hilo kutokana na umuhimu wake ndani na nje ya mipaka ya Jiji la Mwanza.
Mwangi alisema kuwa shindano hilo litasaidia kukuza sekta ya utalii Mwanza na hapa nchini kwa ujumla na pia kuwawezesha wasichana watakaoshiriki kupata ajira kwa ajili ya kuendesha maisha yao.
“Tunaamini mchango unaoletwa na waandaaji wa shindano la Miss Tanzania, kwani unaitangaza nchi vizuri, licha ya kutowahi kutwaa taji la Dunia, ‘Miss World’.
Kwa upande wake, Mratibu wa shindano hilo, John Dotto, alisema kuwa warembo watakaoshiriki shindano hilo, wanatarajia kuingia kambini kuanzia Juni 10 mwaka huu, ambapo wataendelea na maandalizi ya shindano hilo, ambalo linatarajiwa kuwa na msisimko wa aina yake.
Aliwataka warembo wenye sifa za kushiriki shindano hilo waendelee kujitokeza ambapo fomu zinatolewa katika hoteli hiyo ya Gold Crest.
Shindano hilo la Miss Mwanza, linaandaliwa ma Kampuni ya Sisi Entertainment, ambapo mbali na hoteli ya Gold Crest, wadhamini wengine ni Vodacom, Redd’s, PSI, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Fransac General Suppliers.

Comments