MBEYA 'MAPINDUZI STARS YATWAA UBINGWA WA KILI TAIFA CUP 2011

 Naibu Waziri wa TAMISEMI, Kassim Majaliwa, akimkabidhi Kombe la ubingwa wa Michuano ya Kill Taifa Cap mwaka 2011, Kaptani wa timu ya mkoa wa Mbeya, Ivo Mapunda baada ya timu ya mkoa huo kuibuka washindi baada ya kuifunga timu ya mkoa wa Mwanza goli 1-0 wakati wa mchezo wa fainali uliofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Wachezaji na viongozi wa timu ya Mkoa wa Mbeya wakiwa na Kombe la Ubingwa.
Wachezaji wakiwa na Kikombe na mfano wa hundi wa Sh Milion 40 walizokabidhiwa baada ya kutwaa ubingwa huo kwa kuifunga Mwanza bao 1-0 katika fainali.
BAO la dakika ya 88 la mshambuliaji mahiri, mwenye nguvu, Gaudance Mwaikimba,  lilitosha kuipa ubingwa wa Kili Taifa Cup 2011 timu ya Mkoa wa Mbeya ‘Mapinduzi Stars’.
Katika mechi hiyo ya fainali jana kati ya Mbeya na Mwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa, timu zote zilianza kwa kushambuliana kwa zamu, ambapo dakika ya 10, Juma Mpola, aliikosesha Mapinduzi Stars bao kutokana na kukosa umakini, baada ya shuti lake kupaa juu ya lango.
Dakika ya 35, shuti la James Minja wa Mwanza lilitoka nje kidogo ya lango la Mapinduzi. Hadi dakika 45 za kwanza zinakamilika, hakuna timu iliyokuwa imeliona lango la mwenzake.
Kipindi cha pili, kila timu ilichangamka na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara, ambapo dakika ya 60, kipa wa Mwanza, Mweta William, alidaka kwa ustadi faulo ya nje ya 18 ya Gaudance Mwaikimba kabla ya Juma Mpola dakika ya 65 kuwatoka walinzi kadhaa wa Heroes lakini akashindwa kumalizia.
Jerry Tegete wa Mwanza ambaye jana alifichwa vilivyo na mabeki wa Mbeya, naye alikosa bao dakika ya 68 akiwa anatazamana na kipa Ivo Mapunda.
Dakika ya 71, Juma Mpola ambaye alikuwa akitandaza soka ya kuvutia, aliwakosesha tena Mwanza bao, kabla ya mshambuliaji mahiri mwenye nguvu, Gaudance Mwaikimba, kuwanyanyua mashabiki wa Mbeya vitini, baada ya kupachika bao dakika ya 88, baada ya kutokea piga ni kupige katika lango la Heroes na mfungaji kuunganisha wavuni kwa kichwa, bao lililodumu hadi dakika 90 zinakamilika.
Katika mechi hiyo, Ladslaus Mbogo wa Mwanza Heroes alichaguliwa kuwa mchezaji bora na kuzawadiwa kitita cha sh 100,000.
Mwamuzi bora Israel Nkongo, Kocha bora Juma Mwambusi wa Mbeya, Kipa bora Juma Abdul wa Ilala na Mfungaji bora Mwaikimba mwenye mabao manane, ambao wote walijitwalia kila mtu kitita cha sh milioni mbili, huku mchezaji bora wa mashindano akiibuka Juma Mpola wa Mbeya na kuondoka na sh milioni 2.5 huku timu yenye nidhamu ikiwa ni Ilala nayo ikipata sh milioni 2.5.
Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Kassim Majaliwa, alimkabidhi nahodha wa Mbeya, Ivo Mapunda, kombe na kitita cha mfano wa hundi ya sh milioni 40. Washindi wa pili Mwanza walilamba sh milioni 20 huku wa tatu Ilala wakijipatia sh milioni 10.
Kili Taifa Cup 2011 imedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro Premium Lager huku masuala ya habari yakiratibiwa na Executive Solutions.

Comments