TFF, KILIWOOD KUJADILI MUSTAKABALI WA KITUO CHA KUKUZA SOKA KWA VIJANA

Kituo cha kukuza vipaji cha Tanzania Soccer Academy (TSA) kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kampuni ya Kiliwood kimesimamisha shughuli zake tangu mwaka jana.
Kamati ya Utendaji katika kikao chake cha kwanza mwaka huu ilishafanya uamuzi juu ya uendeshaji wa kituo hicho na kutoa maelekezo kwa Sekretarieti ya TFF.
 Kwa vile kituo hicho kilichokuwa kinachukua vijana wenye umri kuanzia miaka 17 hadi 20 ni cha ubia kati ya TFF na Kiliwood uamuzi wowote juu ya mustakabali wake ni lazima uhusishe pande hizo mbili.
Kwa mantiki hiyo Sekretarieti kwa sasa inafanya mawasiliano na kampuni ya Kiliwood ili pande hizo mbili zikutane na kuelezana juu ya uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya TFF juu ya mustakabali wa kituo hicho.
Wajibu wa TFF katika mkataba kati yake na Kiliwood juu ya uendeshaji wa kituo hicho ni vitendea kazi (facilities) ambavyo ni hosteli na uwanja wa mazoezi.

KOZI YA WAKUFUNZI WA MAREFA

TFF kupitia Kurugenzi ya Ufundi imeandaa kozi ya wakufunzi wa marefa wa mikoa itakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Juni 1 hadi 4 mwaka huu.
Kozi hiyo inatarajia kushirikisha wakufunzi wa marefa zaidi ya 20 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara. Mara ya mwisho kozi hiyo ilifanyika nchini mwaka 2008.
Wawezeshaji katika kozi hiyo ni Stanley Lugenge ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Leslie Liunda, Joseph Mapunda, Hafidh Ally na Juma Hamisi.

Boniface Wambura

Ofisa Habari TFF

Comments

Post a Comment