FFU WATAWANYA WANAFUNZI SEKONDARI YA TOSAMAGANGA WALIOKUWA WAKIANDAMANA

 Wanafunzi wa shule ya Sekondari TOsamaganga wilaya ya Iringa wakiandamana kwenda kwa mkuu wa mkoa wa Iringa jana kabla ya kutawanywa kwa mabomu na FFU.


 Wanafunzi wakinyosha mikono juu mbele ya askari wa FFU kuomba wasipigwe mabomu wakati wakijaribu kuandamana bila mafanikio kwenda kwa mkuu wa mkoa wa Iringa.

FFU wakiwazuia wanafunzi wa shule ya sekondari Tosamaganga kuendelea kuandamana bila kibali kwenda kwa mkuu wa mkoa wa Iringa
 
Mwanahabari wa kituo cha Radio Ebony Fm Mark Dolnard akikimbia porini kukwepa kupigwa mabomu na wanafunzi baada ya polisi kuwafukuza waandishi wa habari kuripoti habari za mgomo wa wanafunzi wa shule ya sekondari Tosamaganga (picha zote na Francis Godwin)

Na Francis Godwin, Iringa

HALI ya usalama kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Tosamaganga wilayani Iringa mkoani hapa leo ilikuwa tete baada ya askari wa kikosi cha kutuliza ghasia kulazimika kutumia mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya wanafunzi zaidi ya 1000 wa shule hiyo ambao walikuwa katika maandamano ya amani kuelekea ofisi za mkuu wa mkoa wa Iringa kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya uongozi wa shule hiyo.
Pamoja na askari hao kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi hao kama njia ya kuwazuia wasiandamane bado waandishi wa habari waliokuwepo eneo hilo wakichukua madai ya wanafunzi hao walizuiwa na polisi hao kuendelea kuchukua habari za wanafunzi hao pasipo kibali cha polisi huku wananchi wa maeneo ya Mseke wakizihama nyumba zao kwa muda na kukimbilia porini kukwepa mabomu hayo.
Tukio la mapambano kati ya FFU na wanafunzi hao lilianza majira ya saa 4 asubuhi hadi saa 6 mchana kwa polisi kufukuzana na wanafunzi hao kuwarudisha kwa mabomu shuleni pasipo mafanikio baada ya idadi kubwa ya wanafunzi kukimbilia porini na wengi wao kujificha porini na katika nyumba za wenyeji wa maeneo hayo.
Kabla ya polisi kufika na kuwatawanya wanafunzi hao waliwaeleza waandishi wa habari kuwa sababu ya wao kufanya mgomo wa kutoingia madarasani na kutaka kuandamana kwenda kwa mkuu wa mkoa wa Iringa umetokana na uongozi mbovu wa shule hiyo usiozingatia haki za binadamu.
Waliyataka madai hayo yao kuwa ni pamoja na mfumo wa ufundishaji kutofuata taratibu na kanuni za ualimu ,pia ukosefu wa vitendea kazi kama madawati na vitabu , makamu mkuu wa shule hiyo amekuwa akitumia nafasi hiyo kujinufaisha binafasi badala ya kusaidia kukuza kiwango cha elimu na kuwa amekuwa akidhalilisha wanafunzi kwa kuwapekua simu hadharani hadi kanisani .
Waliwataja walimu wengine zaidi ya 6 wakiwemo wa kike (majina tunayo) ambao wamekuwa wakiwadharirisha kwa kuwapekua sehemu za siri hadharani na kupokonya simu zao kwa faida yao .

Aidha walidai kuwa chakula wanacholishwa shuleni hapo hakina ubora kama wanaoelezwa wazazi huku wakimtaka mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa kutolea ufafanuzi juu ya bajeti inayotengwa shule hiyo kwa ajili ya chakula.
Madai mengine ambayo wanafunzi hao wanapinga ni pamoja na ubadhilifu wa mali za shule pamoja na fedha zinazochangwa na wanafunzi hao .

Walisema kuwa mfano wamekuwa wakichanga rim mbili kwa mwaka rimu zenye thamani ya shilingi 8500 kila moja ila matokeo yake uongozi wa shule hiyo umekuwa ukiziuza rim hizo kwa wafanyabiashara na kununua rim za shilingi 3500 zisizo na ubora kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi hao.

Hata hivyo walipinga matumizi mabaya ya fedha za shule hiyo yanayofanywa na mwasibu na kuwa wana kama wanafunzi wanataka uongozi wa shule hiyo kuweka wazi matumizi ya michango yao mbali mbali ambayo wamekuwa wakichangia .

“Tunatoa pia kujua kuhusu Fund ya wasomi waliosoma hapa Tosamaganga inatumikeje na leo tunaiomba wizara ya elimu ,mkuu wa mkoa wa Iringa ,mkuu wa wilaya ,mkurugenzi na afisa elimu kufika shuleni hapa na kuja kusikia kilio chetu wanafunzi”

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia askari polisi hao wakiongozwa na mkuu wa polisi wilaya ya Iringa (OCD) wakikabiliana na wanafunzi .
Hata hivyo kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Evarist Mangalla alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi aligoma kutoa ushirikiano wowote kwa madai kuwa vyombo vya habari vimeripoti sivyo habari za kutekwa magari juu milima ya Kitonga.Mkuu wa shule hiyo hakuweza kupatikana kuzungumzia madai ya wanafunzi hao kutokana na vikao mbali mbali na vyombo vya dola ambavyo vilikuwa vikiendelea shuleni hapo.

Comments