CCM YAZUA JAMBO UWANJA WA KIRUMBA

                                                     MBUNGE WA ILEMELA, HIGHNESS KIWIA

NA SITTA TUMMA, MWANZA
MBUNGE wa Jimbo la Ilemela Jijini Mwanza, Highness Kiwia (CHADEMA), ametoa muda wa siku 14 (kuanzia jana) kwa uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoani hapa kumlipa fidia ya zaidi ya sh. Mil 50 kwa hasara aliyoipata kuitokana na kutofanyika kwa tamasha la michezo lililowashirikisha wasanii katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.
Amesema kama uongozi wa CCM mkoani Mwanza utashindwa kulipa gharama hizo ndani ya siku hizo, atakwenda mahakamani kuushitaki kwa lengo la kuitafuta haki hiyo kisheria.
Kiwia aliyasema hayo juzi wakati alipokutana na kuzungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Vizano Hoteli Jijini Mwanza, juu ya tamasha la michezo lililowashirikisha wasanii wa Filamu kutoka jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari jijini hapa kwa lengo la kukusanya zaidi ya sh. Mil 30 za kununulia madawati ya shule Jimboni humo.
Alisema, aliandaa tamasha hilo lililofanyika Jumapili wiki iliyopita, na kwamba aliuomba uongozi wa CCM uwanja wa huo utumike katika shughuli hizo kisha kukubaliwa na kulipa sh. 500,000 kama nusu ya gharama ya uwanja huo.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, siku hiyo majira ya saa 5 asubuhi, uongozi wa CCM ulifunga milango na kuzuia watu kuingia uwanjani humo.
"Nasikitika sana CCM kuingiza siasa hata kwenye shughuli za maendeleo kama hizi. Nimeingia hasara kubwa sana kutokana na tamasha hili.
"Kwa maana hiyo, nimemwagiza mwanasheria wangu awape siku 14 kulipa sh. Mil 50 kama gharama zangu, vinginevyo nitawaburuza mahakamani. Haiwezekani niwalipe pesa zangu kisha dakika za mwisho, wanigeuke," alisema Mbunge huyo wa Ilemela.
Akifafanua zaidi, Kiwia alisema siku hiyo watu wengi walijitokeza kwa ajili ya tamasha hilo na hatua ya uongozi wa CCM kuzuia kufanyika kwa tamasha hilo, uliwalazimu wengi wao kurudi majumbani, kabla milango hiyo haijafunguliwa saa 11 jioni.
Alibainisha kuwa, miongoni mwa gharama alizotumia katika kuandaa tamasha hilo la michezo na fedha zake kwenye mabano ni posho za wasanii hao (mil. 6), nauli za ndege kwenda Mwanza na kurudi Dar es Salaam (mil 16), malazi ya wasanii waliotoka Dar es Salaam (720,000), mawasiliano kwa njia ya Posta (300,000), Malipo ya uwanja (mil moja)na gharama za matangazo ni sh. 2,800,000.
Alisema, anaamini CCM walikataa kufungua milango hiyo kwa makusudi, ikiwa ni pamoja na kuhusisha mambo ya kisiasa, anautaka uongozi huo kulipa gharama hizo, kabla hayafungua mashtaka baada ya siku hizo 14 kumalizika.
Kulingana na hali hiyo, alimtaka mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete kukemea viongozi wake wa chini wanaokwamisha maendeleo ya wananchi, kwa kujali itikadi zao za kisiasa.
Mbali ya hayo, mbunge huyo wa Ilemela jijini Mwanza, Kiwia, anatarajia kwenda mahakamani kufungua kesi ya kudai uwanja wa CCM Kirumba uwe ni uwanja wa Umma na fedha zinazopatikana kutokana na gharama za uwanja huo zitumike katika maendeleo ya wananchi, na si kumilikiwa na CCM.
Alisema, anafahamu uwanja huo haukujengwa na CCM, bali ulijengwa kwa nguvu za wananchi, huku baadhi ya watumishi wa umma wakiwa wanakatwa mishahara yao kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa kiwanja hicho, na kwamba haiwezekani CCM ikawa mmiliki pekee chombo cha Umma.
"Pia mimi kwa kushirikiana na wananchi wangu wa Ilemela, tumepanga kwenda mahakamani kuhoji uhalali wa CCM kumiliki uwanja huu. Natambua uwanja huu ulijengwa kwa nguvu ya umma, na si CCM.
"Ni heri uwanja huu uwe chini ya Jiji au wilaya yangu ya Ilemela, na fedha zinazopatikana zitumike kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo ya wananchi", alisema Kiwia, Mbunge wa Ilemela.

Comments