WAAMUZI SITA WA SOKA TANZANIA WAULA CAF




Waamuzi sita wa Tanzania wameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuchezesha mechi za raundi ya kwanza za All Africa Games zitakazochezwa Aprili 30 mwaka huu na Mei 14 mwaka huu. Waziri Sheha akisaidiwa na Hamis Chang’walu na John Kanyenye atachezesha mechi kati ya Malawi na Afrika Kusini itakayochezwa Aprili 30 mwaka huu nchini Malawi.

Judith Gamba akisaidiwa na Saada Hussein na Mwanahija Makame atachezesha mechi ya wanawake kwa michuano hiyo kati ya Zimbabwe na Angola. Mechi itafanyika Mei 14 mwaka huu nchini Zimbabwe. Naye Hafidh Ally ameteuliwa kuwa Kamishna wa mchezo kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Gabon. DRC ndiyo wenyeji wa mechi hiyo itakayochezwa Aprili 30 mwaka huu.

U23 v UGANDA
Mechi ya marudiano ya All Africa Games kati ya timu ya Taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 23 dhidi ya Uganda itakayofanyika Aprili 30 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachezeshwa na Athanase Niyongabo kutoka Burundi.

Waamuzi wasaidizi ambao pia watatoka Burundi ni Jean-Marie Hakizimana na Felix Bazubwabo wakati mwamuzi wa mezani atakuwa Ramadhan Ibada ‘Kibo’ wa Tanzania. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Gaspard Kaijuka kutoka Rwanda.

Boniface Wambura
Ofisa Habari

Comments