TIMU ZOTE 24 ZATHIBITISHA KUSHIRIKI KILI TAIFA CUP 2011

Timu zote 24 zilizothibitisha kushiriki michuano ya Kombe la Taifa mwaka huu (Kili Taifa Cup 2011) zimewasilisha usajili wa wachezaji wao ndani ya mudauliopangwa. Timu hizo na vituo vyao kwenye mabano ni Mtwara, Ruvuma, Kinondoni na Lindi (Lindi).

Nyingine ni Mbeya, Iringa, Temeke na Rukwa (Mbeya), Dodoma, Tabora, Singida naKigoma (Tabora), Arusha, Kilimanjaro, Tanga na U23 (Moshi), Mwanza, Kagera, Mara na Shinyanga (Mwanza) na Pwani, Morogoro, Ilala na Manyara (Morogoro).

Siku ya mwisho kuweka pingamizi kwa wachezaji ni Mei 2 wakati siku ya mwisho kwa Kamati ya Mashindano kuthibitisha usajili ni Mei 3 mwaka huu. Timu zinatakiwa kuwasili vituoni Mei 5 na mashindano yataanza Mei 7.

HAKI ZA TELEVISHENI KILI TAIFA CUP 2011

TFF ilitangaza tenda kwa vituo vya televisheni nchini kuonesha moja kwa moja(live) mashindano ya Kili Taifa Cup. Vituo viwili vya televisheni vilijitokeza kutaka haki ya kuonesha michuano hiyo.

Baadaye kituo kimoja kilijitoa kutokana na sababu za kiufundi wakati kingine kilishindwa kufikia dau ambalo limewekwa na TFF ili kupata haki hizo.

Dau la kuonesha ‘live’ michuano hiyo ni sh. milioni 10. Hivyo hadi sasa hakuna televisheni yenye haki ya kuonesha michuano hiyo.

Bado tunakaribisha vituo vyenye nia ya kuonesha mashindano hayo moja kwa moja kwa mazungumzo. Hivyo tutatoa taarifa baadaye juu ya nini kinaendelea kabla ya mashindano yenyewe kuanza, hasa hatua ya mtoano (knock out).

Boniface Wambura

Ofisa Habari

Comments