TIMU YA TAIFA YA VIJANA CHINI YA MIAKA 23 KWENDA NCHINI UGANDA IJUMAA


Timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 inatarajia kuondoka nchini Aprili 15 mwaka huu kwenda Kampala, Uganda kwa ajili ya mechi ya mchujo ya michezo ya Afrika (All Africa Games) itakayochezwa Jumamosi (Aprili 16 mwaka huu) .

Mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Mandela (Namboole) kuanzia saa 10 kamili jioni itasimamiwa na Kamishna Jean-Didier Masamba Malunga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Waamuzi ni Nur Adbulle, Salah Abukar na Hassan Mohamed kutoka Somalia.

U23 itakuwa na msafara wa watu 30 wakiongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Hafidh Ally Tahir.

Benchi la Ufundi litakuwa na watu sita wakiongozwa na Kocha Mkuu Jamhuri Kihwelo wakati wachezaji ni 20. Timu inatarajia kurejea Dar es Salaam, Aprili 17 mwaka huu.

Mechi ya marudiano itachezwa Aprili 30 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Michuano ya All Africa Games itafanyika jijini Maputo, Msumbiji kuanzia Septemba 3-18 mwaka huu. Timu zimepangwa katika Kanda Saba ambapo mshindi wa kila kanda pamoja na mwenyeji Msumbiji ndiye atakayekwenda kushiriki fainali hizo.

Tanzania iko Kanda ya Tano pamoja na timu za Eritrea, Kenya na Uganda. Iwapo U23 itaitoa Uganda itacheza na mshindi kati ya Eritrea na Kenya. Mechi ya kwanza itachezwa ugenini kati ya Juni 24-26 mwaka huu wakati ya marudiano itakuwa kati ya Julai 8-10 mwaka huu. U23 iko kambini Bamba Beach, Kigamboni ikiwa chini ya Kocha Kihwelo


Boniface Wambura,

Ofisa Habari

Comments