SIMBA,AFRICAN LYON ZAMGOMBEA SAMATTA, KISA DOLA 150,000



KITITA cha dola 150, 000 kilichotoa TP Mazembe kama dau la kumng'oa mshambuliaji chipukizi wa Simba Mbwana Samatta, kimepelekea timu za Simba na African Lyon kumgombea mchezaji huyo kila timu ikidai bi mchezaji wake hali.



Wakati Simba ndiye iliyesimamia zoezi zima la kumuuza mchezaji huyo kwa TP Mazembe, Africnha Lyon imeibuka na kudai kuwa Samatta ni mchezaji wao halali kwani walimpeleka Simba kwa mkataba maalum.



Hata hivyo, Lyon iliandika barua ya malalamiko kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikidai kuwa inastahili kulipwa haki hizo, lakini TFF ilisema kwamba Simba ndiyo inastahili kupata haki hizo kutokana na ukweli kuwa Samatta ni mchezaji wao halali na kama Lyon wana vithibitisho wapeleke.


Ofisa Habari wa African Lyon, Sherally Abdallah, amesema TFF imekiuka taratibu za mkataba wa mchezaji huyo kutoka Lyon kwenda Simba kwani Simba haikufuata taratibu za uhamisho za Samatta na nyota mwingine Rashid Gumbo na licha ya kuwasilisha barua lukuki TFF kudai haki yao bila mafanikio.


Abdallah amesema kuwa kama Samatta si mchezaji wao halali, Novemba 15 mwaka jana, Lyon waliwasilisha barua ya kibali cha maombi ya mchezaji huyo kufanya majaribio katika klabu ya Lisbon ya Ureno, kupitia barua yenye kumbukumbu ALFC/KB/TFF/15-2010, ikieleza majaribio yake yaanze Desemba 3 hadi Januari mwaka huu.


Alisema, Novemba 20, 2010, TFF iliwasilisha barua ya vibali vya Samatta na Hamis Thabit yenye kumbukumbu namba TFF/ADM/Vs-10/32, ikiwatambua ni wachezaji wa African Lyon kwa msimu wa 2010/11.


Abdallah alisema, Julai 21 mwaka jana, viongozi wa Lyon na Simba waliketi katika kikao cha kumaliza tatizo, ambalo ni ulipwaji wa fedha kilichowashirikisha Kassim Dewji, Mohamed Dewji ‘Mo’, Crencentius Magori, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ na Mulamu Ng’ambi ambapo ilikubaliwa uandaliwe utaratibu wa kuwalipa kupitia mechi mbili ambazo ni African Lyon na Simba na ile ya Simba na Yanga, lakini hakuna mafanikio.


Alisema, Desemba 7 mwaka jana waliomba kikao kingine cha suala hilo, lakini hayakupatikana majibu na wakapeleka nakala TFF, ukiachilia mbali pingamizi la wachezaji hao kwa barua iliyowasilishwa Agosti 2, 2010.


Abdallah alisema, kama madai yao hayatafanyiwa kazi wako tayari kupeleka masuala hayo Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

Comments