K-MONDO SOUND YAIBUKA NA KIKOMBE CHA BABU LOLIONDO



Bendi ya muziki wa dansi ya K-Mondo Sound ‘Wazee wa Kibajaji’ wameibuka na rap mpya iitwayo Tukwanywe kikombe kwa babu. Rap hiyo mpya ilianza kutambulishwa Ijumaa iliyopita kwenye ukumbi wa Triz, Mbezi Beach.
Kiongozi wa bendi hiyo, Richard Mangustino alisema rap hiyo pamoja na kutambulishwa kwa mara ya kwanza lakini mashibiki walionekana kuikubali sana jambo ambalo wameamua kuitambulisha sehemu mbalimbali.
“Hii ni rap ambayo niliitengeneza baada ya kuona watu walivyokuwa wakimiminika kwenda Loliondo kupata kikombe kwa mchungaji mstaafu Mwaisapile, hivyo nimewataka watu pia waende Loliondo kupata tiba hiyo na wakija Dar waje K-Mondo kupata furaha za mioyo yao,” alisema.
Mangustino alisema Rap hiyo pia itatambulishwa katika ukumbi wa FK Resort uliopo Mbezi Temboni Jumamosi hii wakati Jumapili, watatumbuiza kwenye ukumbi wa Golden Resort Sinza.
Mbali na Rap ya kikombe cha babu, Mangustino alisema pia watatambulisha nyimbo zao mbili mpya ziitwazo Dodoo na Nelly ambazo zimeonekana kuwashika mashabiki na ambazo zitapelekwa kurekodiwa muda si mrefu.
“Pamoja na rap lakini nyimbo mpya pia zitatambulishwa katika kumbi ambazo tutapiga, naamini mashabiki watakaokuja kutuona watafurahia burudani ambayo tutawapatia, waje wamuone Vumi ambaye atatambulisha pia nyimbo zake mbili mpya nimeumwa kupenda na Afrika,” alisema.
Bendi hiyo inatamba na nyimbo zake za Magambo, Sharufa, Njiwa, Tatizo Umasikini na Kaumia ambazo video zake tayari ziko kwenye vituo mbalimbali vya redio.

Comments