FM ACADEMIA KUZINDUA ALBAMU YA VIDEO YA 'VUTA NIKUVUTE'


Na Mwandishi Wetu

BENDI ya FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma, inatarajia kuzindua video ya albamu ya ‘Vuta Nikuvute’, katika Ukumbi wa Arcade (Heineken House), uliopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, Ijumaa Aprili 29.

Miongoni mwa video zitakazokuwamo katika albamu hiyo ni pamoja na Vuta Nikuvute, Jasmin, Heshima kwa Wanawake na nyinginezo zinazofanya vizuri katika ulingo wa muziki wa dansi hapa nchini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam , Ofisa Habari wa bendi hiyo, Kelvin Mkinga, alisema maandalizi ya uzinduzi wa video hiyo yamekalimika, hivyo kuwataka mashabiki wao waende kwa wingi kujionea burudani hizo.

Alisema kwamba wanachofanya kwa sasa ni kuweka mikakati imara ya kuwapatia heshima zaidi katika muziki wa dansi, kwa kutoa burudani kubwa kwa mashabiki wao katika uzinduzi wa video za albamu ya Vuta Nikuvute.

“Sisi ndio bendi bora kwa sasa kuliko wenzetu, hivyo mipango ni kuwapatia burudani kubwa kutoka kwetu, katika uzinduzi huo, maana tunaamini mashabiki na wadau wetu wanataka raha na sio maneno kama wanavyofanya wengine.

“Naamini hilo litatuweka katika nafasi nzuri ya kuendelea kutamba katika kona ya muziki wa dansi hapa nchini, yenye ushindani wa hali ya juu, ukizingatia kwamba kila mmoja anataka awe juu na kufurahisha watu wake.

Wazee wa Ngwasuma ni miongoni mwa bendi zinazofanya vizuri katika ramani ya muziki wa dansi, huku nyimbo zao nyingi zikionekana kutesa vilivyo hasa ule wa Heshima kwa Wanawake unaozungumzia wanawake.

Comments