FIFA YAISIMAMISHA BOSNIA-HERZEGOVINA


Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) limeisimamisha Bosnia-Herzegovina kuanzia Aprili Mosi mwaka huu baada ya Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la nchi hiyo (FFBH) kutopitisha Katiba yake iliyofanyiwa marekebisho kwa kuzingatia matakwa ya FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ulaya (UEFA).


Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke iliyotumwa kwa wanachama wake, FFBH inapoteza haki zote ilizokuwa nazo kutokana na uanachama wake kwa Shirikisho hilo hadi hapo itakapotolewa taarifa nyingine.


Kutokana na kusimamishwa huko, wanachama wote wa FIFA hawatakiwi kushirikiana na FFBH katika masuala yoyote isipokuwa yale yanayohusu mchezaji binafsi. Hatua hiyo imefikiwa kutoka na uamuzi uliofikiwa Oktoba 28 mwaka jana na Kamati ya Utendaji ya FIFA kuwa FFBH iwe imetekeleza matakwa hayo kufikia Machi 31 mwaka huu.

Boniface Wambura

Ofisa Habari

Comments