EXTRA BONGO KUWAANIKA WAREMBO WA TABATA NA DAR CITY CENTRE SIKU YA PASAKA


Bendi ya Extra Bongo `Next Level’ itatumbuiza kwenye onyesho maalum la kuwatambulisha warembo watakaoshiriki katika mashindano ya Miss Tabata na Miss Dar City Centre siku ya Jumapili ya Pasaka kwenye ukumbi wa Dar West Park , Tabata. Onyesho hilo ambalo linajulikana kama ‘Konyagi Easter Show’, limeandaliwa na Keen Arts na Bob Entertainment chini ya udhamini wa kinywaji cha Konyagi.

Mratibu wa onyesho hilo , Joseph Kapinga alisema kuwa lengo la onyesho hilo ni kuwakutanisha pamoja warembo watakaoshiriki kwenye mashindano ya Miss Tanzania kwenye vituo vya Ilala.

“Tumeamua kufanya hivi ili kuleta changamoto kwa warembo na kufahamiana zaidi kabla hawajashindana kutafuta tiketi ya kwenda Miss Ilala na baadaye Vodacom Miss Tanzania,” alisema mratibu huyo. Warembo wanaoshiriki wanafanya mazoezi kwenye ukumbi wa Dar West na warembo wa Dar City Centre wanaendela kujifua kwenye ukumbi wa Lamada.

Warembo wa vituo vyote wanafundishwa na aliyewahi kuwa Miss Ruvuma 1999, Rehema Uzuia maarufu kama Sweet Ray. Kapinga pia alisema kuwa Extra Bongo watatumia fursa hiyo kuwatambulisha wanamuziki na nyimbo zao mpya kwa wakazi wa Tabata.

Baadhi ya wanamuziki waliohamia bendi hiyo kutoka African Stars `Twanga Pepeta’ ni Rogert Hegga ‘Katapila’, Soul John `Ferguson’, Super Nyamwela, Super Danger, Hosea Mgohachi na Otilia Boniface.

Baadhi ya warembo wanaofanya mazoezi kujiandaa Miss Tabata ni Marion Augustino (18), Neema Marwa (18), Esther Simon (18), Sweetylily Suleiman (21), Malaika Abdallah (18) na Theckler Benedict (19). Wengine ni Happiness Emmanuel (18), Irene Jafari (19), Janeth Marandu (21), Shadya Ally (21), Victoria Amon (20) na Mgayo Salehe (21).

Pia wamo Sarah Hangaya (30), Neema Stanford (21), Upole Athumani (19), Asia Amiri (22), Lucy Paulo (21), Johanita Kanyika (22), Mariamu Lameck (19), Blandina Paul (18), Catherine George (19), Lilian Brayson (24) na Lucia Joseph (20).

Warembo 10 watachaguliwa kwenda kushiriki Miss Ilala na baadaye Vodacom Miss Tanzania. Mrembo anayeshikilia taji hilo ni Consolata Lukosi ambaye katika shindano la ngazi ya taifa mwaka jana alishika nafasi ya tatu na kutwaa taji la balozi wa Redd's, ' Miss Redds Ambassador'.

Comments