COREFA YATUPILIA MBALI RUFAA YA TIMU YA BAGAMOYO FRIENDS

HASSAN OTHAMAN 'HASSANOO', MWENYEKITI WA CHAMA CHA SOKA MKOANI PWANI



Taarifa kwa vyombo vya habari


KAMATI ya Rufaa ya Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Pwani (COREFA), imetupilia mbali rufaa ya timu ya Bagamoyo Friends iliyokuwa ikipinga maamuzi ya Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi iliyotupilia mbali rufaa yao dhidi ya timu ya Maili Moja United ikidai katika mchezo nambari 4, wa fainali ya kombe la Taifa ngazi ya mkoa wa Pwani, uliochezwa Januari 8, mwaka huu, katika uwanja wa Ikwiriri, Rufiji, Maili Moja ilichezesha baadhi ya wachezaji ambao usajili wao haukuzingatia sheria na kanuni za mashindano.

Aidha katika kikao cha kamati hiyo kilichoketi juzi jijini Dar es salaam kuanzia saa 7 mchana hadi saa 5 usiku kikiongozwa na Mwenyekiti Mark Shayo, Makamu wake Joseph Mpuya ambao kitaaluma wote ni wanasheria na katibu Salehe Lubawa, waliitangaza rasmi timu ya Maili Moja United kuwa mabingwa wa soka wa mkoa wa Pwani msimu wa mwaka 2011/12.

Akisoma maamuzi ya kamati saa 5 usiku, Mwenyekiti Shayo alisema sababu zilizoifanya kamati itupilie mbali rufaa ya Baga Friends ni pamoja na barua waliyoiwasirisha katika kamati yake kuwa kama ya pingamizi hivyo, kukosa sifa ya kuwa rufaa halali inayoweza kusikilizwa na kamati yake.

Alisema barua hiyo ilijaa mapungufu ambayo ni pamoja na kutokufuata kanuni ambazo zingeifanya iwe rufani kama inavyoelekezwa na kanuni ya 16 na 17 ya mashindano ya Shirikisho la Vyama vya Soka nchini (TFF).Shayo alisema kamati yake ilizingatia maelekezo ya kanuni ya 16 (C) kwa kuwa barua au rufaa hiyo haikuwa na vielelezo wala haikulipiwa ada hivyo, barua hiyo ni batiri na haikuwa rufaa halali na kamati yake kwa kuzingatia sheria ikalazimika kuitupilia mbali.


Hata hivyo alisema, hatakama rufaa ya Baga Friends ingekuwa halali bado kamati ingeitupilia mbali kwani, maelezo ya barua hiyo yanaelezea kupinga maamuzi ya kamati ya rufaa ya Corefa ambayo haijawai kukaa kujadili na kutoa maamuzi yoyote kuhusu pingamizi ama rufaa yoyote kutoka timu hiyo ya Baga Friends.

Kwa upande wa rufaa ya timu ya Maili Moja, kupinga maamuzi ya kamati ya Nidhamu na usuluhishi kufuta matokeo ya mchezo kati yake na Baga Friends ikidaiwa kuchezesha wachezaji ambao usajili wao haukuwa halali,Shayo alisema kamati yake ilikubaliana nayo.


Alisema katika maamuzi, kamati ilizingatia kanuni ya 34 ya kanuni ya ligi ya taifa ya TFF inayomzuia mchezaji kucheza klabu chochote cha ligi mpaka usajili wake uwe umethibitishwa na chama cha soka ngazi husika ama TFF ambacho kabla ya kumthibitisha mchezaji kitatoa siku 7 hadi 14 kuwasirisha malalamiko ama pingamizi kwa maandishi kuhusu usajili tangu kutangazwa kwa majina ya wachezaji katika klabu husika.

Alisema uthibitisho utakaotolewa na chama ngazi husika au TFF ndio utakuwa wa mwisho na havitapokea rufaa yoyote inayohusu rufaa ya usajili wa mchezaji ambaye hakuwekewa pingamizi mwanzoni isipokuwa, iwapo klabu itafanya udanganyifu kwa jina la mchezaji.


"Baada ya kupitia kanuni ya 34 na ushahidi ulioletwa, kamati yangu iliona kamati ya nidhamu na usuluhishi ilifanya makosa kuipokea na kuijadili rufaa ya Baga Friends kwakuwa haikuletwa mwanzoni kama kanuni hiyo inavyotaka lakini pia, katika maelezo ya kamati hakuna sehemu iliyoeleza kama klabu ya Maili Moja ilifanya udanganyifu wa jina la mchezaji" alisema Shayo.

Baada ya maelezo hayo Shayo kwa niaba ya kamati yake alisema matokeo ya uwanjani yatabaki jinsi yalivyokuwa na ndiyo yatatoa bingwa ambapo Maili Moja ndio walikuwa vinara kwa pointi 9, Big Town wa pili kwa pointi 6, Baga Friends watatu wakiwa na pointi 3 na Black Tiger wakishikiria mkia kwa kumaliza ligi patupu bila kuambulia pointi yoyote.

Comments