YANGA YAACHWA POINTI 4


MABINGWA mara 22 wa Bara tangu mwaka 1965, Yanga, jana walijiweka kwenye nafasi finyu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kutoka sare ya bila kufungana na maafande wa JKT Ruvu katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Katika dakika ya 33, JKT Ruvu walikosa bao la wazi baada ya Kessy Mapande kupata pasi nzuri kutoka kwa Sosteness Manyasi, lakini alishindwa kuitumia.
Jerry Tegete wa Yanga alitumia mkono kuutumbukiza mpira nyavuni dakika ya 42 baada ya kupokea pasi ya Idd Mbaga, lakini mwamuzi David Paul kutoka Kilimanjaro, alikataa kuwa bao.
Dakika mbili baadaye, JKT Ruvu nusura wapate bao lakini shuti la Hussein Bunu ilipanguliwa kiustadi na kipa Ivan Knezevic.
Stephano Mwasyika aliingia ndani ya 18 ya lango la JKT na kukabiliana na kipa Shaaban Dihile, lakini alipatwa na kigugumizi cha miguu na kushindwa kufunga.
Dakika ya 79, Bakar Kondo wa JKT Ruvu alipata nafasi nzuri ya kuweza kufunga baada ya kupata pasi kutoka kwa Mwinyi Kazimoto, lakini alishindwa kuigeuza kuwa bao.
Amos Mgisa alifumua shuti kali dakika ya 84, lakini lilitolewa na kipa wa Yanga, Mserbia, Ivan Kuznevic ambaye alifanya kazi kubwa ya kuokoa michomo ya vijana wa JKT Ruvu chini ya Kocha wake, Charles Kilinda.
Dakika moja baadaye, Athumani Idd ‘Chuji’ aliyekuwa ameingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Nsa Job, aligongana na Erick Majaliwa wa JKT Ruvu na kuumia goti na kushindwa kuendelea na mechi hiyo.
Licha ya Yanga kupambana vilivyo kuweza kushinda walau kufukuzana kwa karibu na mtani wake Simba katika kuwania ubingwa wa ligi hiyo, lakini maafande wa JKT Ruvu nao walionyesha uwezo mkubwa dimbani.
Hadi mwamuzi David Paul kutoka Kilimanjaro anamaliza pambano hilo, kulikuwa hakuna timu iliyopata bao, hivyo Yanga kufikisha pointi 40, ikiwa nyuma kwa pointi nne dhidi ya mtani wake Simba mwenye pointi 44.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Yanga, Sam Timbe aliyeitwaa mikoba ya timu hiyo kutoka kwa Mserbia Kostadin Papic, alisema walikuwa na wakati mgumu kwani licha ya vijana wake kucheza kwa juhudi kubwa, wapinzani wao pia walikuwa wazuri.
Kocha wa JKT Ruvu, Kilinda aliwasifu vijana wake kwa kucheza vizuri huku akiisikitikia Yanga.
“Kiwango cha Yanga bado kipo chini, hakilingani na hadhi, ukongwe na uwezo wao kifedha, wanapaswa kufanya mabadiliko makubwa kwa sababu wana uwezo wa kupata mchezaji kutoka kokote duniani,” alisema Kilinda.
Wakati Yanga ikifikisha pointi 40, hivyo kujiweka kwenye mazingira magumu ya kutwaa ubingwa, JKT Ruvu wao wamefikisha pointi 22, wakiwa nafasi ya saba.
Baada ya mechi ya jana, Yanga imebakisha mechi tatu kabla ya ligi hiyo kufikia tamati hapo Aprili 10; dhidi ya Azam, African Lyon na Toto Africa.
YANGA: Ivan Knezevic, Fred Mbuna, Stephano Mwasyika, Chacha Marwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif, Nsa Job/Athumani Idd ‘Chuji’, Nurdin Bakar, Idd Mbaga, Jerry Tegete na Ernest Boakye/Godfrey Bonny.
JKT Ruvu: Shaaban Dihile, Kessy Mapande, Stanley Nkomola, Shaibu Nayopa, Damas Makwaya, Kisimba Luambano, Nashon Naftar, Mwinyi Kazimoto, Pius Kisambale, Hussein Bunu na Sosteness Manyasi.

Comments