WASHIRIKI SHINDANO LA KISURA 2011 WATAMBIANA

WAREMBO wanaowania taji la Kisura wa Tanzania 2010/11, kila mmoja amejinadi
kuibuka kidedea katika shindano litakalofanyika kesho katika ukumbi wa Hoteli ya
Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam.
Warembo hao walitoa tambo hizo Dar es Salaam juzi, walipotembelea ofisi za
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), zilizopo Ilala, jijini.
Mmoja wa warembo hao, Lethina Christopher, alisema kuwa ingawa miongoni mwao
kila mtu anaonekana kuwa mshindi, lakini hakuna wa kumzidi na kwamba yeye ndiye
atakayeibuka kidedea.
“Nawaomba Watanzania waendelee kunipigia kura namba 20 kuniwezesha kunipa
ushindi,” alisema.
Flaviana Makungwa mshiriki namba 16, alisema: “Nimejiandaa vizuri na najiamini
nina uwezo wa kushinda na kuielimisha jamii yangu na kuweza kuendelea kuitangaza
kampuni yetu ya Kisura.”
Kwa upande wake, Lilian Bussa, mshiriki namba 7, alisema: “Nimejiandaa vizuri
kwa sababu kambini tumepewa mafunzo mbalimbali na mimi naweza kuwa mshindi kwa
sababu nina vigezo vyote vya kuwa mshindi.”
Mshindi wa shindano hilo anayemaliza muda wake, Diana Ibrahimu, aliwataka
washiriki hao kukubali matokeo kwani kwa wale ambao hawatashinda, wajijue kuwa
ni washindi.
Aliwataka wadumishe nidhamu kwa muda wote wanapokuwapo kambini na hata baada ya
shindano hilo ili wawe mfano wa kuigwa kwa jamii.
“Mashindano haya humsaidia mshiriki kujifunza vitu vingi vya jamii na wakitoka
hapa, wanaweza kujitegemea kwa kujiongoza kimaisha,” alisema Diana.
Kwa upande wake, Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Mradi wa Kisura wa Tanzania,
Juliana Urio, amewataka visura wote wazidi kumuomba Mungu kuelekea shindanbo
hilo la kesho na hata wanaporudi katika makazi yao.
Pia, amewataka wazazi kuzidi kuwaruhusu watoto wao kushiriki mashindano hayo kwa
kuwa yana utofauti na mashindano mengine yote ya urembo na uanamitindo kwa
ujumla hapa nchini.
“Nawaomba wazazi wawaruhusu watoto kushiriki katika shindano hili kwa mwaka
unaokuja kwa kuwa mashindano yetu yanamjenga msichana kuweza kujitambua zaidi
katika jamii yake na kuacha utegemezi wa mtu,” alisema Urio.
Mshindi katika shindano hilo litakalosindikizwa na shoo kutoka kwa msanii wa
Bongo Fleva, Shaa, ataondoka na Sh milioni tano pamoja na kuwa balozi wa FHI kwa
mwanza mmoja, huku kukiwa na zawadi nyingine kemkem kutoka kwa wadhamini wa
shindano hilo.
Kisura wa Tanzania 2011 imeandaliwa na BTA na mdhamini mkuu wa shindano hilo
ambalo linafanyika kwa mara ya tatu sasa ni Family Health International (FHI),
wakati wadhamini wengine ni TBL kwa kupitia kinywaji chake cha REDDS, TBC1,
Kiromo View Resort, TanFoam (Arusha), SBC Limited, Flare Magazine, Hugo Domingo,
BASATA, GRM Production, Clouds FM, ATCL, MJ Records, I-View Media, PURE Hair and
Beauty Spa na PURE Academy of Aesthetics.

Comments