THOMAS ULIMWENGU KUJARIBIWA TP MAZEMBE YA DRC


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Machi 8, 2011

Mshambuliaji Thomas Ulimwengu anatarajia kuondoka nchini Machi 11 mwaka huu kwenda Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kufanya majaribio ya kucheza mpira wa miguu wa kulipwa.
Ulimwengu ambaye yuko chini ya wakala wake Damas Ndumbaro anakwenda kufanya majaribio katika timu ya Tout Puissant Mazembe Englebert (TP Mazembe). Ndumbaro ni wakala anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
TP Mazembe ambao ni mabingwa wa Afrika mara mbili mfululizo (2009 na 2010) wana wachezaji wa kulipwa kutoka Zambia na Malawi. Pia timu hiyo ilitwaa ubingwa wa Afrika mwaka 1967 na 1968.
Ulimwengu ambaye yumo kwenye kikosi cha timu ya Tanzania ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 23 (U23) itakayocheza na Cameroon atakuwa kwenye majaribio hadi Aprili Mosi mwaka huu.
Mbali ya kuwa kwenye kikosi cha U23, Ulimwengu yuko kwenye kituo cha mpira wa miguu cha ABC Academy cha Sweden. Pia mshambuliaji huyo amewahi kufanya majaribio katika timu ya daraja la kwanza ya Dalkurd FF nchini humo.
Hata hivyo tunatuma maombi TP Mazembe kama itawezekana baadaye imruhusu mshambuliaji huyo acheze mechi hiyo ya michuano ya Olimpiki. Mechi ya kwanza itachezwa jijini Yaounde, Machi 27 mwaka huu kabla ya timu hizo kurudiana Dar es Salaam wiki mbili baadaye.

TWIGA YASAIDIWA JEZI, MIPIRA
Mpanda baiskeli wa kike Joan Menendez wa Hispania amekabidhi seti mbili za jezi na mipira kumi na moja (11) kwa timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars). Amekabidhi vifaa hivyo leo saa 3 asubuhi kwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara.
Menendez ambaye aliendesha baiskeli kutoka Dar es Salaam hadi Moshi kwa ajili ya kupanda Mlima Kilimanjaro amesema aliiona Twiga Stars alipokuwa Afrika Kusini. Twiga Stars ilishiriki fainali za Afrika zilizofanyika nchini humo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari

Comments