TASWA YAHIMIZA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO KUSHIRIKI TUZO ZA UMAHIRI

BAADHI YA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO
Habari ndugu zangu, naomba kuwakumbusha kuwa Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana an vyama mbalimbali vya kitaaluma vya waandishi wa habari ikiwemo TASWA kimeandaa Tuzo ya Umahiri wa Waandishi itakayofanyika Mei 3, mwaka huu.
Tayari mchakato wa tuzo hiyo umeanza na MCT imetoa fomu kwa wanaohitaji kushiriki katika kila chumba cha habari, naombeni mchukue fomu na mpeleke kazi zenu MCT za mwaka 2010.
Kazi hizo ziwe zile zilizochapishwa katika magazeti ama zilizotangazwa katika redio na televisheni, kuna zawadi nono ni vyema kila anayeona aliandika kazi nzuri ya michezo, ama jamii ama uchumi apeleke MCT mwisho ni Machi 30 mwaka huu.
Kwenye vikao na MCT kuhusu tuzo hizo, watu wa michezo tumekuwa tukielezwa kuwa hatushiriki sana kwenye tuzo, naomba sasa tujitokeze zaidi.
Naamini wengi tunazo makala za kutosha na nzuri zilitoka mwaka jana, tuzipeleke iwe Kiswahili au Kingereza. Pia naombeni kwa maelezo zaidi MCT wanatoa matangazo kwenye magazeti na hata redio na televisheni yatatusaidia kutupa mwanga zaidi wa jambo hili, ama tuwaulize wahariri kwenye vyumba vya habari.
Lingine naomba kuwajulisha kuwa Kamati ya Utendaji ya TASWA itakutana Dar es Salaam kuzungumzia tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Mwaka 2010 itakayofanyika Mei 6 ukumbi wa NSSF.
Pia kikao hicho kitafanya tathmini ya Media Day Bonanza iliyofanyika wiki mbili zilizopita na masuala mengine muhimu yanayohusu chama chetu.
Jambo lingine kama mnavyofahamu viongozi wetu wawili Maulid Kitenge (Makamu Mwenyekiti) na George John (Katibu Msaidizi) wapo Seoul, Korea Kusini kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 74 wa Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS).
Amir Mhando, Katibu Mkuu TASWA

Comments