TAARIFA TOKA TFF


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Machi 11, 2011

UTEUZI WA MENEJA U23
Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Mohamed Adolf ameteuliwa kuwa Meneja wa timu ya Taifa ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 23 inayoshiriki michuano ya mtoano ya Michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwakani jijini London, Uingereza. Pia Adolf kitaaluma na mwalimu wa mpira wa miguu.
U23 ambayo inafundishwa na Jamhuri Kihwelo akisaidiwa na Mohamed Ayoub itacheza mechi ya mchujo ya michuano hiyo dhidi ya Cameroon. Mechi hiyo ya kwanza itachezwa Machi 27 mwaka huu jijini Yaounde. Timu hizo zitarudiana jijini Dar es Salaam wiki mbili baadaye.
Mchujo wa mwisho katika kikosi cha U23 kilichopo kambini hoteli ya Bamba Beach, Kigamboni utafanyika Machi 13 ili kubaki na wachezaji 25. Kikosi hicho hivi sasa kina wachezaji 32. Timu inatarajiwa kuondoka Machi 23 mwaka huu kwenda Yaounde.
TFF inafanya mawasiliano na timu za Azam na Mtibwa Sugar ili zicheze mechi za kirafiki na U23. Pia mawasiliano bado yanaendelea na Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) ili timu yao ya U23 ije nchini kucheza mechi ya kirafiki na U23 kabla ya safari ya Yaounde.

TIMU YA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Timu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo Machi 27 mwaka huu itacheza mechi ya mchujo ya Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) dhidi ya Taifa Stars itakuja nchini na msafara wa watu 32 utakaoongozwa na Waziri wa Michezo wa nchi hiyo Aurelien Zingas. Kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Jamhuri ya Afrika ya Kati (FCF) msafara huo utakuwa na wachezaji 23 watakaokea Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Gabon, Ufaransa, Morocco, Congo Brazzaville na Singapore.
Wachezaji hao ni Prince Samola, Delphin Gbazinon, Audin Boutou, Nicaise Ozingoni, Mamadi Saoudi, Hilaire Momi, Geoffroy Lembet, Euloges Enza, Manasse Enza, Foxi Kette-Vouama, David Manga, Habib Habibou, Josue Balamandji, Fernander Kassai, Salif Keita, Freddy Lignanzi, Amores Dertin, Eudes Dagoulou, Vianney Mabide, Charly Dopekoulouyen, Emmanuel Yezzouat, Onassis Kemo na Franklin Anzite.
Boniface Wambura
Ofisa Habari

Comments