SIMBA YAIMARISHA BENCHI LA UFUNDI KWA KUONGEZA MAKOCHA 2, LENGO NI KUHAKIKISHA WANAIFUNGA TP MAZEMBE APRILI 3


WAKATI mechi ya marejeano ya Ligi ya mabingwa baina ya Simba na TP Mazembe ikitarajiwa kupigwa Aprili 3 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Wekundu wa Msimbazi wameimarisha benchi lake la ufundi kwa kuongeza makocha wawili.
Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, alisema, hatua hiyo inatokana na umuhimu wa mechi hiyo, ambayo wanahitaji kushinda mabao 2-0 ili kusonga mbele.
Alisema, katika kujiimarisha huko, wamemuongeza mkurugenzi wa ufundi wa timu ya vijana ya Simba, Abdallah ‘King’ Kibadeni, kuwa msaidizi wa kocha mkuu, Patrick Phiri, pamoja na Amour Awadh kutoka Oman ambaye atakuwa ni kocha wa makipa.
Aliongeza kuwa kutokana na Phiri kuwa nyumbani kwao Zambia akiuguliwa na mkewe, kwa sasa benchi la ufundi litakuwa chini ya Kibadeni, ambaye atasaidiana na Amri Saidi na pindi atakaporejea, Kibadeni atakuwa chini ya Mzambia huyo.
“Phiri alikuwa na matatizo ya kifamilia tangu tukijiandaa na mechi yetu na AFC, lakini kutokana na kukabiliwa na mechi na TP Mazembe ilibidi aendelee kuwepo, huenda akawasili leo, lakini kwa kipindi hiki Kibadeni ndiye ataliongoza benchi la ufundi,” alisema.
Rage aliongeza kuwa maandalizi ya mechi hiyo yanakwenda vema na kushinda mabao mawili inawezekana, hivyo amewaomba Watanzania kwa ujumla kuipa sapoti timu ili iweze kuhamasika na kucheza kwa nguvu zote.
“Kama tuliweza kuivua ubingwa Zamalek mwaka 2003, kwa nini tusiweze kuiondoa TP Mazembe? Mimi nadhani hilo linawezekana, tunahitaji sapoti ya Watanzania wote, kwani Simba inaiwakilisha Tanzania,” alisema.
Katika hatua nyingine, Rage alisema waamuzi wa mechi hiyo wanatarajiwa kutoka nchini Shelisheli, huku kamisaa atatoka Kenya na wameishafanya taratibu za kuwatumia tiketi kama zinavyoelekeza kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Comments