SIMBA BINGWA 99%


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Bara, Simba, jana walizidi kuchanja mbuga kuelekea kwenye ubingwa wa ligi hiyo iliyoanza Agosti 21, mwaka jana baada ya kuifyatua AFC Arusha mabao 2-0 katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini hapa.
Ushindi huo umeiwezesha Simba kuzidi kung’ara kileleni mwa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 44, na kutengeneza tofauti ya pointi nne dhidi ya mshindani wake mkubwa, Yanga.
Ingawa lolote linaweza kutokea, yatosha kusema uwezekano wa Simba kutetea ubingwa wake, ni asilimia 99 kwa kuzingatia idadi, aina ya mechi zilizosalia, uwezo pamoja na ari.
Wakati Simba ikisaliwa na mechi tatu dhidi ya Kagera Sugar, JKT Ruvu na Majimaji, Yanga wao wamebakisha dhidi ya Azam FC, timu ngumu inayopigania nafasi ya pili kama si ubingwa ili kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao, African Lyon na ndugu zao Toto Africa ya Mwanza.
Kama timu hizo watani wa jadi zitashinda mechi zao zilizosalia, Simba itafikisha pointi 53 na Yanga 49, hivyo uwezekano wa Wekundu wa Msimabzi kutwaa ubingwa ni mkubwa zaidi.
Katika mechi ya jana iliyokuwa gumzo kubwa tangu katikati ya wiki, Simba iliyotia mguu katika jiji hili Alhamisi, walikuwa wa kwanza kuziona nyavu za AFC katika dakika ya tano, likifungwa na Patrick Ochan.
Ochan, nyota wa kimataifa wa Uganda alifunga bao hilo kiustadi akiumalizia mpira uliotemwa na kipa Emmanuel Makungu kufuatia shuti la Emmanuel Okwi na kuamsha shangwe na nderemo.
Licha ya wenyeji AFC chini ya Kocha wake Rashid Chama kupambana vilivyo, lakini dakika ya 12, walijikuta wakipachikwa bao la pili lililofungwa na Rashid Gumbo kwa shuti kali la nje ya maguu 18.
Mabao hayo yaliwaamsha AFC na kuanza kulisakama lango la Simba, lakini licha ya kuwepo kwa kosa kosa nyingi, hadi filimbi ya mapumziko wageni walikuwa mbele kwa mabao hayo mawili.
Dakika ya 85, Abdallah Juma aliyeingia kipindi cha pili, nusura aifungie timu yake bao, lakini kipa Juma Kaseja alionyesha umahiri na kuokoa.
Licha ya juhudi hizo za wenyeji AFC kutaka kusawazisha na pengine kupata ushindi walau kujiokoa na hatari ya kushuka daraja, hadi mwamuzi Thomas Mkombozi anamaliza pambano hilo, Simba ambao ni mabingwa mara 17 wa Bara tangu 1965, walitoka kifua mbele kwa mabao 2-0.
Kabla ya mechi hiyo, visa na vibweka vilitawala huku mechi ikibeba taswira kama ya fainali ya kuamua timu itakayotwaa ubingwa wa ligi hiyo itakayofikia tamati Aprili 10.
Tangu Simba ilipofika mjini hapa Alhamisi usiku, joto la mechi hiyo lilianza kusambaa kwa kasi kwa wanachama wa Simba kuanza kujipanga kusaka mbinu za ushindi huku AFC nao wakisaidiwa na wanachama wa Yanga kuhakikisha wanashinda.
Juzi, baadhi ya wanachama na viongozi wa Tawi la Yanga Arusha walionekana wakiwa katika vikao vya hapa na pale na wakizunguka hadi katika kambi ya Simba iliyokuwa
eneo la Kaloleni na kuwatia hofu mashabiki wa Simba.
Aidha, kabla ya mechi hiyo ya jana, kulikuwa na utata mkubwa kuhusu viingilio kwani baada ya kumalizika kikao cha maandalizi ya mchezo jana saa tano, meneja wa uwanja alitangaza kuwa ni shilingi 10,000 kwa jukwaa Kuu na mzunguko shilingi 5,000.
Mashabiki walianza kupinga wakisema ni vikubwa ukilinganisha na mchezo wenyewe na kutolea mfano mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga kiingilio cha chini kilikuwa shilingi 3,000.
Mzozo mkubwa ulizuka pale baadhi ya wasiopenda usumbufu kuamua kukata tiketi hizo na kukutwa Jukwaa Kuu imeandikwa tiketi sh 5,000 na mzunguko tiketi zake zimeandikwa sh 3,000.
Hali hiyo iliwafanya mashabiki waliokuwa wamefika tangu saa tano asubuhi, kujazana katika milango ya kuingilia bila kukata tiketi wakipinga viingilio hivyo.

Comments

  1. Dina tunahiaji kushinda mechi 2 tu hiyo ya mwisho hata tukifungwa tunakuwa mabingwa tu kwani tutakuwa tumepoteza point 3

    ReplyDelete

Post a Comment