POULSEN ATAKA WACHEZAJI STARS KUJITUMA ILI KUFUNGA AFRIKA YA KATI JUMAMOSI


KOCHA mkuu wa timu ya taifa ya soka Tanzania, ‘Taifa Stars’, Jan Poulsen, amewataka wachezaji wake kujituma ipasavyo na kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo wa keshokutwa dhidi ya Afrika ya Kati unaotarajiwa kupigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jijini Dar es Salaam , Poulsen aliwataka wachezaji wake kujituma na kutambua kuwa Watanzania wanawategemea kushinda katika mchezo huo.
Poulsen alisema kutokana na mazoezi aliyowapa wachezaji wake, ana matumaini ya kuifunga Afrika ya Kati, japokuwa baadhi ya wachezaji wanaokipiga nje ya Tanzania wataukosa mchezo huo.
Aliwataja nyota hao ambao hawatakuwepo kutokana na timu zao kutowaruhusu kuwa ni pamoja na Nizar Khalfan anayekipiga Canada, Danny Mrwanda na Abdi Kassim walioko Vietnam.
Aidha Poulsen aliwataja wachezaji wanaocheza nje ya nchi waliojiunga na kikosi chake kuwa ni pamoja na Idrissa Rajab anayekipiga Sofapaka ya Kenya, Athuman Machupa anayecheza Sweden na Henry Joseph Kongsvinger ya Norway.
Poulsen, aliwataka wachezaji waonyeshe uzalendo katika mchezo huo, sambamba na Watanzania pia wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu yao.
Kwa upande wake, Nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa alisema, wamejiandaa vilivyo kwa ajili ya mchezo huo na watayatumia vilivyo mafunzo ya Kocha Poulsen.
Naye kocha wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Accorsi Julies, alisema, mchezo una matokeo matatu, lakini wao wamejipanga kushinda kesho.
Julies alisema, kikosi chake kimejipanga vilivyo kwa ajili ya mchezo huo, kwa sababu vijana wake wana ari ya kushinda mchezo wa kesho.
Katika hatua nyingine, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), jana ilikabidhi hundi ya sh milioni 100 kwa Katibu Mkuu wa TFF, ikiwa ni sehemu ya mkataba wao wa kuidhamini Stars, ambazo zitatumika katika maandalizi ya timu hiyo.

Comments