NCHUNGA, MOSHA KUWEKWA KITI MOTO KESHO

NCHUNGA KUSHOTO NA MOSHA
MWENYEKITI wa matawi ya Yanga Mkoa wa Dar es Salaam, Mohammed Msumi ameitisha mkutano wa viongozi wa matawi utakaofanyika kesho kuanzia majira ya saa 8 mchana makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Kariakoo.
Kwa mujibu wa Msumi, lengo la mkutano huo ambao utahudhuriwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga na Makamu wake, Davis Mosha, ni kujadili mustakabali wa klabu hiyo.
Alisema, agenda kubwa itakuwa kujadili sababu za kujiuzulu kwa Mosha, huku akitakiwa kutoa ufafanuzi wa kina mbele ya viongozi wa matawi, kwa lengo la kunusuru mpasuko mkubwa unaoinyemelea klabu hiyo.
Msumi alisema, katika kikao hicho, Nchunga na Mosha wakiwa waalikwa kwa mujibu wa nafasi zao, hivyo kubeba dhamana kubwa ya klabu hiyo, kila mmoja atajieleza kuhusu hali ilivyo katika klabu hiyo.
“Ndiyo nikiwa Mwenyekiti wa matawi ya Yanga Mkoa wa Dar es Salaam, nakiri hali ya mambo katika klabu yetu si shwari, kwa sababu pale juu (uongozi), hapajatulia kabisa na ndio maana mambo hayaendi,” alisema Msumi.
Alisema, kwa lengo la kunusuru hali ya mambo kuharibika zaidi, Mosha ameitwa kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu sababu za kujiuzulu kwake, kwani kama hali hiyo itaondelea, kuna hatari uongozi mzima ukapukutika.
Msumi alisema baada ya Mosha kutoa ufafanuzi wake, Nchunga naye atatoa maelezo yake kuhusu hali ya mambo inayoukabili uongozi wake ulioingia madarakani Julai 18, mwaka jana.
Alisema, kinachosikitisha ni kuona kila kukicha, uongozi wa klabu yao umezidi kutikiswa, hivyo ni muhimu kwa viongozi wa matawi kujadili kwa kina chanzo na hali hiyo kwa lengo la kupata ufumbuzi.
Msumi alisema, kama viongozi wa matawi wataona suala hilo linapaswa kufikishwa kwa wanachama, wataitisha mkutano mkuu kwa lengo la kuinusuru klabu hiyo hata kama yatakuwa maamuzi magumu.
Alisema, ingawa kuna kila dalili za Yanga kuukosa ubingwa kwa mwaka wa pili mfululizo, ni muhimu kusawazisha mambo, kwa sababu mbali ya ligi, klabu inakabiliwa na mambo mengi ya msingi ukiwamo usajili kwa ajili ya msimu ujao.
Hatua hiyo ya wanachama imekuja huku Mosha akiwa ametangaza kujiuzulu kutokana na matatizo yaliyopo kwenye uongozi hadi hali ya mambo kwenda ndivyo sivyo huku Nchunga akilaumiwa kwa udhaifu.

Comments