KUMEKUCHA MAONYESHO YA PILI YA MAVAZI YA HARUSI


Maonyesho ya mavazi ya kwanza na ya kipekee yanatarajiwa kuanza kurindima mwanzoni mwa mwezi ujao kuanzia tarehe 1 mpaka 3 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam , huku maandalizi ya maonyesho hayo kwa mwaka huu yakiwa yamekamilika yakiwa na washiriki zaidi ya 51 waliothibitisha kushiriki. “mwaka huu tuna washiriki mbalimbali na toka sehemu tofauti wakiwemo kutoka Arusha na Zanzibar , hii ni kuthibitisha tu kwamba maonyesho haya sasa ni ya kitaifa zaidi na si Dar es salaam tu” alisema Mustafa Hassanali, muaandaaji wa maonyesho hayo. Kama ilivyokuwa kwa maonyesho ya mwaka jana , siku ya pili kwa mwaka huu itakuwa ni kwa wabunifu mbalimbali na wauzaji wa magauni ya Harusi kuonyesha mavazi yao katika Maonyesho ya nguo za Harusi, ambapo hii itaanza saa mbili usiku. Kwa kweli hii si ya kukosa kwa wale wanaotarajia kufunga ndoa. “mwaka huu tumeongeza kipengele kipya cha Mdahalo wa Harusi ambapo wataalamu na waliobobea katika mambo mbalimbali ya Harusi watatoa mada, hii ni pamoja na kuzungumzia yanayopasa katika Harusi, urembo, jinsi ya kuchagua mavazi ya Harusi, keki, mapambo, bila kusahau yahusuyo wanaume katika Harusi. Hii ni pamoja na kuwaleta pamoja wahusika wa Harusi, wataalamu, na kupata habari toka kwa wenye utaalam wa masuala hayo hapa nchini.” Aliongezea kusema Hassanali. “kwa siku tatu za maonyesho ya Harusi kwa mwaka huu, milango itakuwa wazi kuanzia saa 4 asubuhi kila siku mpaka saa 2 usiku, na tunawaomba sana wadau na watarajiwa wa Harusi kutembelea maonyesho ya mwaka huu, na kuonyesha ushirikiano kwa wajasiriamali wetu nchini.” Alimalizia kusema Mustafa Hassanali. Maonyrsho ya Harusi kwa mwaka huu yamedhaminiwa na Clouds FM, Daily News, Habari Leo, Global Outdoor Systems, Image Masters, Ultimate Security, Vayle Springs, Eventlites na 361 degrees.

Comments